Leo, tarehe 07 Novemba 2023, Mheshimiwa Balozi Baraka Luvanda ametembelewa na Balozi wa Hiari wa Utalii Tanzania, Bw. Nicholaus Reynolds, almaarufu, Bongozozo aliyeambatana na binti yake Jesca na wawakilishi wa Diaspora wa Tanzania waliopo Japan.
Bongozozo yuko katika ziara ndefu ya kikazi katika Bara la Asia ambapo, kabla ya kuja Japan alitembelea Ufilipino, Cambodia, Indonesia, Singapore, Thailand na Taiwan.
Mara baada ya salamu na maelezo mafupi ya ziara yake, Bw. Nicholaus (Bongozozo) alimshirikisha Balozi Luvanda dhamira yake ya kushirikiana na Ubalozi, kuleta wanariadha wa Tanzania kwenye Mashindano ya Marathon ya Tokyo (Tokyo Marathon) yanayotarajiwa kufanyika jijini Tokyo, Japan mnamo mwezi Machi 2024.
Bw. Nicholaus (Bongozozo) alishukuru kwa ukarimu na mapokezi mazuri aliyoyapokea Ubalozini na kutoka kwa watanzania waliopo nchini Japan tangu kuwasili kwake Japan tarehe 27 Oktoba 2023 na alieleza kuwa anaelekea jijini Kyoto kutalii kabla ya kurejea Uingereza.
Aidha, binti yake Jesca alieleza kuwa kwa sasa anasomea Shahada ya Umahiri ya Mambo ya Kale (Masters in Archeology) nchini Uingereza; na baadaye ana dhamira ya kufanya Shahada ya Uzamivu (Phd.) kwenye eneo hilo. Lengo lake ni kuwa aje kuwa mbobezi kwenye mambo ya kale ya Tanzania.
Kwa upande wake Balozi Luvanda alimshukuru na kumpongeza Bw. Nicholaus (Bongozozo) kwa namna anavyochangia kwa kiasi kikubwa katika kutangaza utalii, lugha ya Kiswahili na utamaduni wa mswahili ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
Vilevile, Balozi Luvanda alimuhakikishia Bw. Nicholaus ushirikiano wa Ubalozi wa wakati wote na kumuahidi kushirikiana naye katika kutimiza dhamira yake ya kuleta wanariadha wa Tanzania kwenye Mashindano ya Tokyo Marathon, hapo mwakani.
Balozi Luvanda alihitimisha kwa kumtambulisha mgahawa unaomilikiwa na mtanzania uliopo Kyoto ambapo, alimshauri autembelee atakapokuwa Kyoto. Baada ya maongezi Balozi Luvanda alimkaribisha Bongozozo kupata chakula cha mchana yeye pamoja na ujumbe alioambatana nao.









