Tarehe 26 Agosti 2023, Balozi Baraka Luvanda aliungana na Mabalozi wengine wa Nchi za Afrika zenye uwakilishi nchini Japan katika Hafla ya Maadhimisho ya Miaka 30 ya Jukwaa la Kimataifa la Tokyo la Kujadili Maendeleo ya Africa (TICAD) iliyoandaliwa na Serikali ya Japan kupitia Wizara ya Mambo ya Nje. Hafla hiyo ilihudhuriwa na washiriki takriban 400 kutoka Serikali ya Japan, Balozi za Nchi za Afrika nchini Japan; wanasiasa; makampuni binafsi na ya umma; asasi za kiraia; na mashirika ya maendeleo.
Akifungua hafla hiyo, Waziri Mkuu wa Japan, Mhe. Fumio Kishida alieleza kuwa Japan imekuwa mshirika mkubwa na wa karibu wa Afrika kupitia jukwaa la TICAD kwa kipindi cha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993. Alieleza kuwa, kwa miaka ijayo TICAD itaendelea kufungua fursa za maendeleo na usalama barani Afrika; na kubainisha kuwa kuimarisha uhusiano na mataifa ya Afrika ni mkakati na kipaumbele kikubwa kwa Taifa la Japan.
Aidha, Waziri Mkuu Kishida alielezea matumaini yake ya kuendelea kushirikiana na mataifa ya Afrika katika kuendeleza Jukwaa la TICAD ikiwemo, Mkutano ujao wa TICAD 9 unaotarajiwa kufanyika jijini Yokohama mnamo mwaka 2025. Vilevile, alitoa wito kwa mataifa ya Afrika kushirikiana na Japan katika maandalizi na ushiriki kwenye Maonesho ya Biashara ya Dunia ya Osaka (OSAKA EXPO) ambapo, Japan ni mwenyeji. Maonesho hayo ya Dunia yanatarajiwa kufanyika tarehe 13 Aprili hadi 13 Oktoba 2025, jijini Osaka.
Hafla hiyo ya Miaka 30 ya TICAD, ilijumuisha pia maonesho mbalimbali ya shughuli za uwekezaji zinazotekelezwa na kampuni za Japan barani Afrika; iliyofanyika sanjari na uwepo wa semina maalum kuhusu historia, tathmini na mwenendo wa TICAD kwa mataifa ya Afrika na Japan, iliyotolewa na jopo la wanasiasa, wanadiplomasia, wasomi, wawakilishi wa sekta za umma na binafsi, na mashirika ya maendeleo yakiwemo, JICA, UNDP na UNIDO.
Waziri Mkuu wa Japan, Mhe. Fumio Kishida akifungua Mkutano wakati wa Hafla ya Maadhimisho ya Miaka 30 ya TICAD jijini Tokyo, tarehe 26 Agosti 2023
Waziri Mkuu wa Japan, Mhe. Fumio Kishida akifungua Mkutano wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Miaka 30 ya TICAD jijini Tokyo, tarehe 26 Agosti 2023
Naibu Katibu Mkuu wa Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa-UNDP na Mkurugenzi wa Masuala ya Afrika, Bi. Ahuna Eziakonwa, akitoa hotuba wakati wa Hafla ya Maadhimisho ya Miaka 30 ya TICAD iliyofanyika jijini Tokyo

