Tarehe 30 Septemba 2023, Ubalozi ulishiriki kwenye Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Miaka 50 ya Chuo Kikuu cha Tsukuba iliyofanyika chuoni hapo, jijini Ibaraki, Japan. Balozi Luvanda alikuwa miongoni mwa wageni rasmi walioalikwa katika hafla hiyo ambapo, alipata fursa ya kusalimiana na kubadilishana mawazo na viongozi mbalimbali wa chuo hicho pamoja na vyuo vikuu vingine vya Japan vilivyoalikwa kwenye hafla hiyo.

Ushiriki wa ubalozi kwenye maadhimisho hayo, ni kwa minajiri ya kuimarisha mahusiano mazuri baina ya Tanzania na Chuo Kikuu cha Tsukuba pamoja na kuongeza mtandao wa kutafuta fursa za masomo kwa watanzania nchini Japan. Watanzania wengi wanaendelea kunufaika na elimu katika Chuo Kikuu Tsukuba chini ya Mpango wa Ufadhili unaotolewa na Chuo Kikuu hicho.

Katika barua ambayo ubalozi umemuandikia Rais wa Chuo Kikuu cha Tsukuba kumshukuru kwa mwaliko na kwa ukarimu siku ya maadhimisho hayo, ubalozi umeelezea dhamira ya kuanzisha mashirikiano kati ya Chuo Kikuu hicho na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.