Tarehe 30 Disemba 2022, Balozi Baraka Luvanda alishiriki katika ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka 2022 wa Umoja wa Wanafunzi wa Kitanzania walioko Japan (TSJ) uliofanyika katika mji wa Fukuoka, Japan. Mkutano huo ulijumuisha Viongozi na wajumbe wote wa Umoja huo wakiwemo watanzania wengine wachache walioalikwa kwenye ufunguzi.
Katika hotuba yake, Mwenyekiti wa Umoja aliyemaliza awamu ya uongozi, Bi. Eunice Likotiko alirejea shukrani zake kwa Mheshimiwa Balozi Baraka Luvanda kwa kukubali dhamana ya kuwa mlezi wa Umoja na pia kwa kuitendea haki nafasi hiyo ndani ya kipindi cha mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa Umoja huu. Bi. Likotiko alielezea Faraja yaw ana-TSJ kuona ubalozi ukiwa bega kwa bega nao na hivyo kuwa sehemu ya mafanikio makubwa ya TSJ ndani ya kipindi cha mwaka mmoja. Vile vile, alimshukuru Balozi Luvanda kwa kuweza kutenga muda wake kushiriki katika Mkutano wa Pili wa TSJ.
Baada ya salamu hizo za utangulizi, Bi. Likotiko alitumia fursa hiyo kuwasilisha taarifa ya utendaji ya TSJ ya mwaka 2021/2022 ambapo, Pamoja na mambo mengine, alibainisha mafanikio na changamoto ambazo Umoja umezipitia katika kipindi husika. Alielezea kuwa baadhi ya mafanikio ambayo TSJ iliyafikia na inajivunia ni pamoja na: Kuongeza idadi ya wanachama mara tatu zaidi ya awali na kufanya idadi yao kuwa 60 hadi sasa; kufanya kazi kwa karibu na Ubalozi wa Tanzania nchini Japan na Ubalozi wa Japan nchini Tanzania; na kuitangaza TSJ katika vyombo mbalimbali vya habari na kuwafikishia watanzania wengi taarifa kuhusu fursa mbali mbali za masomo na mafunzo kwa ufadhili zinazopatikana nchini Japan na kuwasaidia namna ya kuziomba . Alieleza kuwa wamefanikisha jambo hili kwa kutumia mitandao mbali mbali ya kijamii, machapisho mbali mbali n ahata mahojiano na baadhi ya vyombo Habari, televisheni na redio.
Hata hivyo, Bi. Likotiko alielezea kuwa Pamoja na mafanikio hayo kumekuewpo na baadhi ya changamoto na akazitaja kuwa ni pamoja na ; uchache wa nafasi za ufadhili wa masomo kwa Watanzania kutoka Serikali ya Japan ukilinganisha na nchi nyingine ;kushindwa kuzifikia kirahisi taasisi za elimu nchini ili kuweza kuziunganisha na taasisi za elimu za Japan zenye hamasa ubwa ya kuingia katika Makubaliano (MoUs) ya ushirikiano ambao alieleza kuwa ni wa manufaa makubwa na, kukosekana kwa mawasiliano ya pamoja ya wanafunzi waliowahi kusoma nchini Japan miaka iliyopita (alumni), jambo ambalo alisema wanakusudia kuanzisha mtandao wa alumni wa Japan kwa ajili ya kusaidiana na kushauriana na kuifanya TSJ iwe bora zaidi.
Akihitimisha hotuba yake, Bi. Likotiko aliwatambulisha Viongozi wapya wa TSJ waliochaguliwa tarehe 29 Disemba, 2022 ambao wataongoza kwa muda wa mwaka mmoja (1). Viongozi waliotambulishwa walikuwa ni: Bi. Gloriana Monko, Mwenyekiti; Bw. Zuberi Zavuga, Makamu Mwenyekiti; Bw. Innocent Calist Mramba, Katibu; Bw. Almachius Mutasigwa, Naibu Katibu; na Bw. Changoma Francis, Mweka Hazina.
Mwisho, Bi. Likotiko alishukuru kwa mara nyingine kwa ushirikiano mkubwa ambao Balozi na Maafisa wake wamekuwa wakiwapatia viongozi wanaomaliza muda wao na kuomba ushirikiano uendelee kwa viongozi wapya ili kuifanya TSJ iwe imara na yenye mafanikio zaidi.
Kwa upande wake, Balozi Luvanda aliwashukuru Uongozi wa TSJ kwa kumwalika ili aweze kushiriki katika Mkutano wa Pili wa Mwaka. Aidha, aliwapongeza viongozi waliohitimisha awamu ya uongozi kwa mafanikio makubwa na kuwapongeza Viongozi wapya kwa kuchaguliwa kushika nydhifa hizo adhimu na akawatia shime shime kuendeleza umoja huu na kuuimarisha zaidi.
Balozi Luvanda alielezea Faraja yake kuona kuwa katika safu ya uongozi mpya angalau kuna wa zamani akisisitiza kuwa upo umuhimu wa waliokuwepo kusaidia kumbukumbu (institutional memory) ya taasisi yoyote ile.
Vile vile, Balozi Luvanda alielezea kufarijika kwake kwa mafanikio ya umoja huu ndani ya kipindi cha mwaka mmoja na kwamba ushirikiano uliojengwa baina ya wanachama ni wa manufaa sio tu wa kielimu bali pia kijamii. Kadhalika, aliwapongeza Viongozi na wanaumoja wote kwa ujumla huo kwa kutumia fursa mbalimbali kuitangaza nchi yetu kupitia vyombo vya habari na kushiriki katika matukio na maonesho mbalimbali ambako wamekuwa wakipeperusha vema bendera ya Tanzania nchini Japan.
Balozi Luvanda aliipongeza TSJ kwa kazi nzuri ya malezi kwa wanajumuiya wapya kila wanapoingia nchini Japan. Akarejea kutoa rai aliyoitoa mwaka jana (2021) ya kuwataka wana-TSJ kuendelea kuwa wageni wazuri nchini Japan kwa kutii bila shuruti sheria za wenyeji ambapo, kwa kufanya hivyo watakuwa wamedumisha sifa nzuri ya Tanzania.
Akihitimisha, Balozi Luvanda aliwahakikishia wana-TSJ kuwa milango ya Ubalozi iko wazi wakati wote na kwa aina yoyote ya huduma itakayohitajika na kwamba Ubalozi utaendelea kushirikiana na umoja huo bega kwa bega katika kutekeleza mipango ya umoja huo; kuendeleza; na kubuni mipango mipya kwa pamoja na kushirikiana kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazojitokeza.
Baada ya hotuba hiyo, Balozi Luvanda alipewa jukumu la kuwakabidhi vyeti vya utumishi uliotukuka viongozi waliomaliza awamu ya uongozi ambapo, aliwakabidhi vyeti hivyo viongozi wafuatao; Bi. Eunice Likotiko - Mwenyekiti; Bw. Innocent Mramba - Katibu; Bi. Johari Mengi - Mweka Hazina; Bw. Elias Balimponya - Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba; Bw. Anwar Ahmed Salim - Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Kijamii; Bw. Joram Ntiyakunze - Mwenyekiti wa Kamati ya Ufadhili; na Bi. Suzan Kessy - Mwenyekiti wa Kamati ya Habari na Mawasiliano.


