Shindano la 32 la Hotuba kwa Lugha ya Kiswahili la Kuwania Kombe la Mwasisi wa Chuo Kikuu Soka, Tokyo Japan lilifanyika tarehe 27 Novemba 2022 katika Chuo Kikuu Soka ambapo Mheshimiwa Balozi Baraka Luvanda alialikwa kuwa Mgeni Rasmi na Jaji wa shindano hilo.
Shindano hilo lililoandaliwa na Klabu ya Urafiki ya Pan African (Pan African Friendship Society) ya Chuo Kikuu Soka lilibeba kauli mbiu isemayo “Ufunguo wa Dunia yenye amani umo kiganjani mwako”.
Washiriki wa shindano hilo waliwasilisha mada kwa lugha ya Kiswahili zilizolenga kauli mbiu hiyo zilizokuwa na ujumbe wa umuhimu wa kudumisha amani duniani. Baada ya mawasilisho hayo, walipatikana washindi watatu waliozawadiwa zawadi mbalimbali kutoka kwa waandaji wa shindano pamoja na Balozi za Nchi za Afrika Mashariki ambapo Kiswahili kinazungumzwa na wengi.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa shindano hilo, Mhe. Balozi Luvanda alielezea namna ambavyo Kiswahili kimekuwa kikitumika nchini Tanzania kama kielelezo cha utamaduni wa Mtanzania na pia kiungo muhimu katika kudumisha amani na umoja wa Taifa la Tanzania, tangu kupatikana kwa uhuru wake.
“Tanzania ni nchi yenye watu takribani milioni 61 na makabila yapatayo 120 ambayo yametawanyika sehemu mbalimbali za nchi wenye kuzungumza lugha za kikabila zaidi ya mia moja na ishirini, kwa kuwa kila kabila lina lugha yake. Hata hivyo, Kiswahili ndiyo lugha ya Taifa na asilimia 90 ya watanzania wanaizungumza nchini kote: labda, mtapenda pia kujua kuwa Kiswahili kinazungumzwa na takriban watu milioni 500 duniani” alibainisha.
Aidha, Balozi Luvanda alitumia fursa hiyo kutoa rai kwa jamii ya Japan kupenda kuizungumza na kuitangaza lugha ya Kiswahili ili iendelee kutambulika zaidi Japan ambapo kwa sasa imepewa heshima ya kuwa na siku yake maalumu ya kuadhimishwa duniani kote. Aliendelea kueleza kuwa mnamo mwezi Novemba 2021, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) lilitangaza kuwa tarehe 7 Julai ya kila mwaka ni Siku ya Kiswahili Duniani na hivyo hatuna budi kuienzi na kuidumisha lugha hiyo adhimu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Shindano hilo, Bi. Nozomi Tanaka wa Klabu ya Urafiki wa Pan African ya Chuo Kikuu Soka, akitoa salamu za shukrani alielezea namna Mwasisi wa Chuo Kikuu Soka, Dkt. Daisaku Ikeda alivyovutiwa na Afrika hadi kupelekea kuanzisha kwa mashindano hayo kwenye miaka ya 1990.
Bi. Tanaka alitumia fursa hiyo pia kuwashukuru washiriki na wahusika wote wa Shindano la 32 la Hotuba kwa lugha ya Kiswahili na kueleza kuwa hotuba za washiriki kwa mwaka huu zinalenga Waafrika wenye mioyo isiyoshindwa inayoweza kuongoza ulimwengu kudumisha amani. Aliongeza kuwa kwa kipindi hiki ambacho dunia inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo, machafuko ya kivita, amani inapaswa kuhubiriwa kwa watu wote.
Kabla ya kuanza kwa shindano hilo la Kiswahili, Balozi Luvanda alipata fursa ya kufanya mazungumzo na Makamu Mkuu wa Chuo Soka, Prof. Akio Nishiura ambapo mazungumzo yao yalijikita zaidi katika kuanzisha program za ushirikiano baina ya vyuo vikuu vya Tanzania na Chuo Kikuu Soka.








