Tarehe 18 Septemba 2022, Balozi Baraka Luvanda amezindua na kukabidhi jezi kwa Timu ya Mpira wa Miguu ya Watanzania waishio Japan (The Kilimanjaro FC) ikiwa ni hatua ya kutimiza ahadi yake aliyoitoa wakati alipotembelewa na timu hiyo Ubalozini mnamo tarehe 3 Julai 2022.
Katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania waishio Japan (Diaspora - inayojulikana kwa jina la Tanzanite Society) Bw. Frank Semaganga, aliyeambatana na Nahodha wa Timu ya Kilimanjaro FC, Bw. Felix Fred pamoja na wachezaji wa timu hiyo walipokea jezi iliyopambwa kwa vivutio mbalimbali vya utalii wa Tanzania ikiwemo, Mlima Kilimanjaro kama lilivyo jina la timu hiyo.
Hafla ya kukabidhi jezi ya timu iliambatana pia na uzinduzi wa Mashindano ya Mpira wa Miguu yajulikanayo kama “The Tanzanite Festival” ambayo ilisindikizwa na michezo ya kukata na shoka iliyohusisha timu za Kilimanjaro FC, Nigeria All Star, Shonan Sri Lanka na ICS Vietnam.
Mashindano ya The Tanzanite Festival yanatarajiwa kufanyika kila mwaka na kushirikisha timu za mpira wa miguu za Diaspora kutoka nchi mbalimbali zenye uwakilishi nchini Japan.




