Tarehe 3 Julai 2022, Balozi Baraka Luvanda alipokea Ubalozini, Timu ya Mpira wa Miguu ya Watanzania waishio Japan inayojulikana kwa jina la “Kilimanjaro Football Club”. Timu hiyo ikiwa chini ya uongozi wa Kapteni wa Timu, Bw. William F. Felix iliwasilisha vikombe vya ushindi ulioupata katika mashindano ya mpira wa miguu yaliyofanyika; tarehe 12 Disemba 2021, Kombe la International Support Center na kuibuka mshindi wa pili; na tarehe 22 Mei 2022, Kombe la Lanka ambapo waliibuka mshindi wa tatu.
Akiwasilisha vikombe hivyo, Bw. Felix, alielezea historia fupi ya timu hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2019 hadi sasa ambapo wamefanikiwa kushiriki katika mashindano kadhaa ya mpira wa miguu kwa Diaspora yanayoandaliwa nchini Japan. Alieleza kuwa ushindi wa hivi karibuni ni wa tatu na kwamba timu hiyo ilishawahi kuwa mshindi wa kwanza kwenye mashindano ya Kilimanjaro Futsal Super Cup yaliyofanyika tarehe 25 Oktoba 2020. Akaeleza kuwa mashindano hayo ya 2020, yaliandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Japan.
Aidha, Bw. Felix alielezea matarajio ya timu hiyo na changamoto wanazokumbana nazo katika kufikia malengo ya timu waliyojiwekea. Akaeleza kuwa changamoto kubwa ni kutokuwa na jezi maalumu ya timu pamoja na usafiri. Hivyo, aliomba kurejea ombi lao kwa Ubalozi ambalo waliwasilisha wakiomba kusaidiwa kupatikana kwa jezi ya timu.
Kwa upande wake, Balozi Luvanda aliwapongeza sana kwa ushindi mkubwa walioupata katika mashindano hayo ambao umeiletea heshima pamoja na kuitangaza Tanzania kupitia michezo hiyo. Aidha, aliwasisitiza kuendeleza juhudi wanazofanya katika kuitangaza nchi na kuwaomba kuendelea zaidi kuvitangaza vivutio vyake hapa Japan; na kwamba kwa kufanya hivyo watathibitisha uzalendo na mapenzi makubwa waliyonayo na nchi yao Tanzania.
Balozi Luvanda aliwakumbusha wajibu wao wa kutii sheria na taratibu za nchi ya Japan ambayo wao ni wageni kwani kutokutii sheria kunaleta sifa mbaya sio tu kwa jamii ya Watanzania waishio Japan bali kwa Taifa la Tanzania, kwa ujumla.
Balozi Luvanda alihitimisha mazungumzo yake na timu hiyo kwa kuwaahidi ushirikiano wa Ubalozi kwa timu hiyo; na pia kwa jamii nzima ya Watanzania waishio Japan. Alimalizia kwa kutoa ahadi ya kusaidia kutatua changamoto ya jezi ambayo alipendekeza kuwa ipambwe kwa vivutio mbalimbali vya utalii wa Tanzania ikiwemo, Mlima Kilimanjaro kama lilivyo jina la timu hiyo.








