Tarehe 20 Machi 2023, Balozi Baraka Luvanda alikutana na kufanya mazungumzo na Viongozi wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Tanzania wanaosoma nchini Japan “Tanzanian Students Association in Japan – TSJ”.  Viongozi hao ni Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Bi.Gloriana J. Monko na Katibu wa Jumuiya Bw. Inocent Calist.

Katika mazungumzo yao, Viongozi hao walitoa shukrani zao kwa Balozi Luvanda ambaye ni mlezi wa jumuiya hiyo kwa namna wanavyopata ushirikiano kutoka ubalozini kuhusiana na masuala mbalimbali ikiwemo kushiriki katika uchaguzi wa viongozi wa Jumuiya hiyo uliofanyika 29 Disemba 2022 na mkutano wao wa mwaka 2022 uliofanyika tarehe 30 Disemba 2022, katika mji wa Fukuoka.

Mwenyekiti alieleza mikakati waliyonayo ambayo utekelezaji wake unategemea ushirikiano na ubalozi kuwa ni pamoja na kuongeza idadi ya fursa za masomo kwa watanzania nchini Japan zikiwemo, Shahada ya Kwanza (undergraduate), kutafuta fursa za programu za kubadilishana uzoefu wa wataalam wa sekta mbalimbali toka Japan na Tanzania na malengo waliyonayo ya kuisajili jumuiya hiyo ili iweze kutambulika kwa mamlaka za Japan.

Kwa upande wake, Balozi Luvanda aliwashukuru Viongozi hao kwa mipango mizuri waliyonayo ambayo kwa kiasi kikubwa inaendana na utekelezaji wa majukumu ya ubalozi.  Alieleza jitihada mbalimbali zinazofanywa ili kuongeza nafasi za ufadhili wa masomo kwa watanzania nchini Japan zikiwemo, za shahada ya kwanza suala ambalo lilishafikishwa kwa Serikali ya Japan na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa alipofanya ziara nchini Japan mwezi Septemba, 2022 na ubalozi utaendelea kufuatilia utekelezaji wake. Kuhusu usajili wa Jumuiya hiyo kwa mamlaka za Japan, alisema kuwa suala hilo litafanyiwa kazi ili kuona namna ya kulitekeleza. Alihitimisha kwa kuwashukuru kwa kazi nzuri wanayofanya kuwaunganisha wanafunzi na kuwaahidi ushirikiano wakati wote.