Tarehe 11 Oktoba 2014, Tanzania imeshiriki na kuhitimisha kwa mafanikio makubwa Maonesho ya Kimataifa ya Kahawa nchini Japan ya mwaka 2024 (2024 Japan Speciality Coffee Conference & Exhbition) yaliyofanyika jijini Tokyo, kuanzia tarehe 9 Oktoba 2024. Tanzania imeendelea kuitangaza kahawa inayozalishwa nchini kupitia Maonesho hayo ambapo, imeonekana kuvutia wahudhuriaji wengi.
Maonesho haya, ni fursa adhimu katika kukuza soko la kahawa ya Tanzania nchini Japan ambayo ni kahawa pendwa iliyopewa jina maarufu la kibiashara la “Tanzania Kilimanjaro Coffee”. Jina hili hutumika nchini Japan, kwa kahawa zinazozalishwa Tanzania pekee, kwa kutambua kivutio kikubwa cha Mlima Kilimanjaro uliopo nchini Tanzania.
Tanzania inasifika Japan kwa kutoa kahawa bora aina ya Arabica (Arabica laini - full washed na Arabica ngumu - natural) inayolimwa katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Mara, Tanga, Morogoro, Njombe, Iringa, Katavi, Rukwa, Ruvuma, Kigoma, Songwe na Mbeya; na kahawa ya Robusta inayolimwa mkoani Kagera.