Tarehe 18 Mei 2023, Ubalozi kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) na UNIDO Tokyo uliandaa Kongamano la Kwanza la Uwekezaji mahsusi kwa ajili ya kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini kwa wawekezaji kutoka Japan. Takriban washiriki wapato 250 kutoka makampuni ya Japan walishiriki Kongamano hilo la Kwanza na la aina yake lililofanyika kwa njia ya mtandao.
Taasisi za Tanzania zikiwemo, Ofisi ya Rais – Uwekezaji, Wizara ya Viwanda na Biashara, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) zilishiriki Kongamano hilo. Washiriki wengine ni Ubalozi wa Japan nchini Tanzania, JICA na baadhi ya kampuni za Japan zilizowekeza Tanzania. Kampuni hizo ni Matoborwa Co. Ltd na Saint Parts Co. Ltd ambazo, zilipata fursa ya kuelezea uwekezaji wao nchini Tanzania na kuwahamasisha wawekezaji wengine wa Japan.
Balozi Baraka Luvanda katika hotuba yake alitoa rai kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa Japan kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini Tanzania hususan, kwenye maeneo ya kimkakati kama vile, uwekezaji katika utalii, nishati, madini, kilimo, viwanda, uchumi wa buluu. Alitumia fursa hiyo kuelezea sababu mbalimbali za kuwekeza nchini Tanzania zikiwemo: uwepo na amani na utulivu wa kisiasa; mazingira bora ya kuvutia uwekezaji; jiografia ya nchi na mipaka yake; na uwepo wa huduma za msingi na miundombinu kama maji, umeme, barabara, reli, usafiri wa ndege na huduma za simu na mtandao nchi nzima.
Kongamano hilo lilikuwa na mawasilisho mbalimbali kutoka kwa Balozi wa Japan nchini Tanzania, Mhe. Yasushi Misawa; Mkurugenzi wa Uwekezaji kutoka Ofisi ya Rais Uwekezaji, Bw. Chilumba; Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania, Bw. Gilead Teri; Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Viwanda la Umoja wa Mataifa, Ofisi za Tokyo Bi. Fumio Adachi; na Mkurugenzi Mwakilishi wa Ofisi ya JICA Tanzania, Mr. ARA Hitoshi.
Mawasilisho hayo yalifuatiwa na majadiliano kuhusu uwekezaji nchini Tanzania ambapo, pia kulikuwa na nafasi ya maswali na majibu. Washiriki hao waliipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji kwa jumla. Aidha, walishukuru kwa kupata uelewa mpana kuhusu Tanzania na fursa za uwekezaji zilizopo.
Taarifa zaidi, tafadhali tembelea http://www.unido.or.jp/news/13579/
