Balozi wa Tanzania nchini Japani Mheshimiwa Anderson Mutatembwa amesema watanzania 23 wanaoishi katika Mkoa wa Kumamoto Kusini mwa Japani, uliokumbwa na tetemeko la ardhi hivi karibuni wako salama.
Balozi Mutatembwa amesema hayo leo alipokutana na kufanya mazungumzo na Bwana Fredrick Nwaka, Mtaalamu mpya wa Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Umma la Japan, NHK.
Nwaka amejiunga na NHK akitokea Shirika la utangazaji Tanzania, TBC.
Mazungumzo hayo yamefanyika katika ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Japani zilizopo eneo la Setagaya.
Balozi Mutatembwa amesema Ubalozi wa Tanzania nchini Japani umekuwa na mawasiliano ya karibu na watanzania hao ambapo 13 ni wanafunzi wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kumamoto.
Katika mazungumzo hayo Balozi Mutatembwa pia amemkaribisha Nwaka nchini Japani na kumhakikishia ushirikiano wa karibu kwa muda wote atakaofanya kazi nchini Japani.
Hali kadhalika Balozi Mutatembwa amemtaka Nwaka kushirikiana na Ubalozi kutangaza fursa mbalimbali za Tanzania nchini Japani ikiwemo Jukwaa la uwekezaji litakalofanyika mwezi Septemba na ambalo litahudhuriwa na taasisi mbalimbali kutoka sekta binafsi na za umma kutoka Tanzania.



