Leo, tarehe 15 Februari 2024, Balozi wa Tanzania nchini Japan, Mhe. Baraka Luvanda alipokea msaada wa magari ya zimamoto na uokoaji kutoka Serikali ya Japan. Magari hayo yalikabidhiwa na Bw. Goda Katsuaki ambaye ni Naibu Mkurugenzi Mkuu Masuala ya Kimataifa wa Taasisi ya Zimamoto ya Japan - “Japan Firefighters Association (JFA)”.
Katika makabidhiano hayo, Balozi Luvanda ameishukuru serikali ya Japan kwa kuendelea kuisaidia Tanzania katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo. Aidha, Bw. Goda alisema taasisi hiyo itaendelea kutoa msaada wa magari hayo ya zimamoto pamoja na magari ya kubeba wagonjwa kwa njia maombi ya moja kwa moja au kwa utaratibu wa Official Development Assistance (ODA).
Magari hayo yaliyopatikana yanatarajiwa kusafirishwa hivi karibuni kwenda Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Tanzania kwa ajili ya kuhudumia wananchi.




