Tarehe 25 Januari 2023, Balozi Luvanda alifanya mkutano na Makamu wa Rais wa JICA, Bw. ANDO Naoki kwenye Makao Makuu ya Shirika hilo jijini Tokyo. Katika mkutano huo, Bw. Naoki aliambatana na Bi. SUZUKI Momoko, Mkurugenzi wa masuala ya Afrika; Bw. ARA Hitoshi, Mkurugenzi Mwakilishi wa Ofisi ya JICA Tanzania; Bw. OKUMOTO Masakatsu, Mkurugenzi Msaidizi wa masuala ya Afrika; na Bw. FUJIWARA Shunsuke, Afisa anayeshughulikia masuala ya Tanzania.
Akielezea lengo la ujio wake, Balozi Luvanda alimshukuru Bw. Naoki kwa kukubali ujio wake na akamweleza kuwa ujio huo unalenga kufuatilia yatokanayo na Mkutano wa Nane wa Kilele wa TICAD (Eighth Summit of Tokyo International Conference on African Development – TICAD 8) uliofanyika mwezi Agosti 2022, Tunisia; na Ziara ya Kikazi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa iliyofanyika mwezi Septemba 2022 nchini Japan.
Balozi Luvanda alimueleza Bw. Naoki kuwa kabla ya kukutana naye, alifanya mazungumzo na Balozi Saida Shinichi, Mkurugenzi Mkuu wa Masuala ya Afrika wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Japan mnamo tarehe 17 Januari 2023; hivyo baadhi ya masuala atakayozungumza naye, yalishawasilishwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Japan kupitia Mkurugenzi huyo.
Baada ya kuwasilisha lengo la ujio wake, Balozi Luvanda aliishukuru JICA na Serikali ya Japan kwa ujumla wake kwa ushirikiano mzuri kati ya Tanzania na Japan uliodumu tangu mwaka 1961 baada ya Shirika hilo kufungua ofisi zake nchini kwa mara ya kwanza. Alieleza ushirikiano huo umewezesha Tanzania kupokea misaada ya kitaalam, mikopo ya masharti nafuu na misaada kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
Aidha, Balozi Luvanda alirejea wito uliowasilishwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa Waziri Mkuu Kishida wa Serikali ya Japan kuzingatia kuongeza idadi ya wanafunzi wa kitanzania wanaonufaika na programu ya ufadhili ya ABE na programu zingine 9 za masomo zinazotolewa kuwawezesha watanzania kupata ujuzi katika masuala mbalimbali. Alimueleza Bw. Naoki kuwa kupitia mazungumzo ya viongozi hao, Tanzania pia iliomba ufadhili zaidi katika masuala ya utabibu, uhandisi na TEHAMA; na kuangalia uwezekano wa kufadhili masomo ya shahada ya kwanza kwa watanzania.
Vilevile, Balozi Luvanda alikumbushia ombi la Tanzania la kukamilishwa utekelezaji wa miradi ya Tanzania iliyowasilishwa kwenye mikutano ya TICAD 6 na TICAD 7; na ombi la ufadhili wa miradi mipya iliyowasilishwa kwenye TICAD 8. Alirejea rai iliyotolewa na Waziri Mkuu Majaliwa kwa Kampuni ya TOSHIBA ya utekelezaji wa Mradi wa Uendelezaji Nishati ya Umeme wa Jotoardhi. Aliiomba JICA kuangalia uwezekano wa kuwezesha ukamilishwaji wa miradi hiyo ya TICAD; na kufadhili miradi ya umeme inayotokana na vyanzo tofauti ukiwemo, Mradi wa Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa Kutumia Gesi Asilia wa Mtwara – MW 300 (Mtwara Thermal Power Plant).
Balozi Luvanda alihitimisha maelezo yake kwa kutoa wito wa kurejesha Programu Maalum ya Mafunzo ya Uongozi (OSAKA Special Training Program) inayotolewa JICA. Alielezea manufaa ya programu hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000 ambapo imeweza kuibua maarifa na fikra mpya kwa washiriki kwa kuchota uzoefu wa Japan na kuutumia katika kuboresha Sera za Tanzania za uongozi hususan, kwenye ngazi ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa. Kutokana na umuhimu huo, Balozi Luvanda alitoa rai kwa JICA kuiendeleza programu hiyo ili watanzania wengi zaidi waweze kunufaika nayo.
Kwa upande wake Bw. Naoki, alishukuru Balozi Luvanda kwa ujio wake na wasilisho alilolitoa ambapo alimuahidi kuwa ofisi yake itafuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa miradi iliyowasilishwa kwenye mikutano ya TICAD. Aidha, alifafanua kuwa utekelezaji wa Mradi wa Mtwara Thermal Power Plant utailazimu JICA kuingia ubia na wadau wengine wa maendeleo; na kuhusu programu ya Osaka, alieleza kuwa watafuatilia kufahamu sera na vipaumbele vya sasa vya Tanzania kuhusu utekelezaji wa programu hiyo.







