Waziri Mkuu Khasim Majaliwa, kwenye picha ya pamoja na Viongozi wengine Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika, kwenye Mkutano wa TICAD 8 uliofanyika Tunis, Tunisia mwezi Agosti, 2022
Waziri Mkuu Khasim Majaliwa, akiwa kwenye mazungumzo na Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida, wakati wa Ziara ya Kikazi nchini Japan, Mwezi Septemba, 2022

Tarehe 13 Januari 2023, Balozi Luvanda alifanya mkutano na Balozi Saida Shinichi, Mkurugenzi Mkuu wa Masuala ya Afrika wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Japan kwenye Ofisi za Wizara hiyo jijini Tokyo. Lengo la mkutano huo lilikuwa kufuatilia yatokanayo na Mkutano wa Nane wa Kilele wa TICAD (Eighth Summit of Tokyo International Conference on African Development – TICAD 8) uliofanyika mwezi Agosti 2022, Tunisia; na Ziara ya Kikazi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa iliyofanyika mwezi Septemba 2022, nchini Japan. 

Akizungumza katika mkutano huo, Balozi Luvanda aliishukuru Serikali ya Japan kwa uhusiano mzuri wa kidiplomasia na wa kidugu uliojengeka kwa muda mrefu tangu Tanzania ilivyopata uhuru wake, mwaka 1961. Uhusiano huo uliouwezesha Tanzania kutekeleza miradi yake kimaendeleo pamoja na programu mbalimbali za kukabiliana na kupunguza umaskini. Alieleza kuwa kupitia uhusiano huo mzuri, Tanzania inamuangalia Japan kama mdau mkubwa katika maendeleo yake ya kiuchumi.

Aidha, Balozi Luvanda alimkumbusha Balozi Shinichi kuhusu maombi ya Serikali ya Tanzania yaliyowasilishwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa Waziri Mkuu Kishida wakati wa Mkutano wa Uwili uliofanyika pembezoni mwa TICAD 8 na ule uliofanyika wakati wa Ziara ya Kikazi nchini Japan. Alibainisha kuwa Tanzania iliiomba Japan kuzingatia kuongeza idadi ya wanafunzi wa kitanzania wanaonufaika na programu ya ufadhili ya ABE na programu zingine 9 za masomo zinazotolewa na Serikali ya Japan kwa vijana kupata ujuzi katika masuala ya kilimo, uvuvi, utawala, elimu ya fedha, madini na usafirishaji. Alieleza kuwa Tanzania iliomba ufadhili zaidi katika masuala ya utabibu, uhandisi na TEHAMA; na kuomba kuangaliwa kwa uwezekano wa kufadhili masomo ya shahada ya kwanza. 

Balozi Luvanda pia alirejea wito wa Serikali ya Tanzania wa kuanza tena kwa mazungumzo juu ya mikataba ya kodi (Double Taxation Avoidance Agreements -DTAA) na mikataba ya kulinda uwekezaji (Bilateral Investment on Promotion and Protection Agreement – BIPA) kati ya Tanzania na Japan. Alirejea ahadi ya Waziri Mkuu Majaliwa kwa Waziri Mkuu Kishida kuwa Tanzania ipo tayari kurejesha mazungumzo ya kuhuisha mikataba hiyo, iliyokwama kukamilika tangu mwaka 2018. 

Vilevile, Balozi Luvanda alikumbushia suala la kuhitimishwa kwa Programu Maalum ya Mafunzo ya Uongozi (OSAKA Special Training Program) inayotolewa na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA). Alieleza kuwa tangu kuanzishwa kwa Programu hiyo mwaka 2000, imeweza kuibua maarifa na fikra mpya kwa washiriki kwa kuchota uzoefu wa Japan na kuutumia katika kuboresha Sera za Tanzania za uongozi hususan, kwenye ngazi ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa. Kutokana na umuhimu wa programu hiyo, aliwasilisha ombi la kuiendeleza programu hiyo iliyodumu kwa miaka 22 ili watanzania wengi zaidi waweze kunufaika kwayo. 

Balozi Luvanda alihitimisha maelezo yake kwa kuishukuru Serikali ya Japan kwa kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ukiwemo, Mradi uliozinduliwa karibuni wa Uendelezaji wa Soko la Samaki la Malindi na Vituo vya Uuzaji wa Samaki, Zanzibar ambapo Rais na Mwenyekiti wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi alilizindua tarehe 10 Januari 2023. 

Kwa upande wake Balozi Shinichi, alishukuru kwa ujio wa Balozi Luvanda na namna ambavyo Serikali ya Tanzania inatambua mchango wa Japan katika kuendeleza miradi ya maendeleo ya Tanzania. Balozi Shinishi alimhakikishia Balozi Luvanda kuwa Ofisi yake imeyapokea masuala yote yaliyobainishwa katika mazungumzo hayo na kuahidi kuyawasilisha kwenye mamlaka husika za Japan.