Tarehe 18 – 19 Oktoba 2023, Mheshimiwa Balozi Baraka Luvanda amefanya ziara ya kikazi ya siku mbili katika miji ya Matsuda na Odawara jijini Kanagawa. Ziara hiyo iyoratibiwa na Bw. Suzuki Koji, Rais wa Kampuni ya K.K Suzuki kwa kushirikiana na Ubalozi ilianzia katika Mji wa Matsuda na kumalizikia Mji wa Odawara.
Katika ziara hiyo, Balozi Luvanda alipokelewa na wenyeji wake ambao ni: Bw. Hiroyuki Motoyama, Meya wa Mji wa Matsuda na Bw. Masato Tamaki, Naibu Meya wa Mji wa Odawara. Katika Mji wa Matsuda, ziara hiyo ilijumusha: Kutembelea Ofisi ya Meya wa Matsuda; kutembelea eneo la kupumzika watu la Nishidaira (Nishidaira Park); na kutembelea Shule ya Msingi ya Matsuda. Katika Mji wa Odawara, ziara ilijumuisha kutembelea: Kituo cha kusafisha na kusambaza maji katika mji wa Odawara (Odawara City Water Bureau); kampuni ya Suzuhiro Kamaboko inayotengeneza umeme kwa kutumia nishati jadidifu na kusindika chakula cha baharini; Shule ya Msingi ya Kanrei Shirayuri Gakuen; na Makumbusho ya Hakone Art.
Aidha, tarehe 18 Balozi Luvanda alipata fursa ya kujumuika kwenye chakula cha jioni na Mstahiki Meya Motoyama ambapo walipata fursa ya kuzungumza masuala mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano kati ya Mji wa Matsuda na Tanzania.
Kwa ujumla ziara hii ilikuwa ya mafanikio makubwa kwa kuwa Viongozi wa Miji hii miwili wameonesha nia yao ya dhati ya kutaka kuanzishwa mashirikiano na miji pamoja na shule za Tanzania kwa ajili ya maendeleo ya maoneo husika. Katika mazungumzo baina ya pande hizi mbili, imependekezwa kufanyike ziara nyingine mahsusi kwa ajili ya kujifunza masuala ya kilimo katika miji hiyo na kwa upande wa Tanzania kueleza kwa kina fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini.
Vilevile, katika upande wa Elimu uongozi wa Miji hiyo pamoja na shule zilizotembelewa wamekuwa na shauku ya kufahamu zaidi kuhusu shule zilizopo Tanzania na zaidi kutaka kuanzisha mahusiano na shule zilizopo nchini ili kuweza kubadilishana taarifa na ujuzi.
Balozi Luvanda amewahakikishia kuwa ziara hii ni mwanzo wa kuanzishwa kwa mahusiano baina ya Tanzania na miji hii kwamba Ubalozi utafanya ziara za mara kwa mara ili kuimarisha mahusiano hayo na hatimaye kuanzisha ushirikiano kupitia uhusiano wa Miji Dada (Sistership- Cities).
Picha ya Pamoja ya Balozi na Meya wa Matsuda, Timu ya Wamama walioandaa hafla ya chai ya kijapan pamoja na Maafisa Ubalozi katika eneo la kupumzika watu la Nishidaira (Nishidaira Park).
Picha ya Pamoja ya Balozi na Meya wa Matsuda, Bw. Hiroyuki Motoyama, Mkuu wa Bodi ya Elimu ya Matsuda, Bw. Kazuyuki Josen, Bw. Suzuki Koji, Bw. Greyson Ishengoma na Bw. Kazuma Shirai kutoka Balozi wa Tanzania wakiwa katika Shule ya Msingi ya Matsuda.
Picha ya Pamoja ya Balozi na Naibu Meya wa Mji wa Odawara, Bw. Masato Tamaki, Bw. Suzuki Koji na Maafisa Ubalozi katika Ofisi ya Kituo cha Kusafisha na Kusambaza maji cha Mji wa Odawara
Balozi Luvanda akitoa hotuba fupi kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Kanrei Shirayuri Gakuen
Balozi Luvanda kwenye picha ya Pamoja na Wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Kanrei Shirayuri Gakuen
Balozi Luvanda katika Picha ya Pamoja na Wanafunzi waliompokea alipowasili kwenye Makumbusho ya Hakone Art Pamoja na Mwalimu wao.
