Balozi Baraka Luvanda akipokelewa na Balozi Ian McConville, Mkuu wa Itifaki wa Jumuiya ya Madola ya Australia.
Balozi Baraka Luvanda akisaini kitabu cha wageni katika Ofisi ya Gavana Mkuu wa Jumuiya ya Madola ya Australia.
Balozi Baraka Luvanda akitambulishwa na kusalimiana na Mke wa Gavana Mkuu Hurley.
Balozi Baraka Luvanda kwenye picha ya pamoja na Mheshimiwa David John Hurley, Gavana Mkuu wa Jumuiya ya Madola ya Australia.

Tarehe 28 Machi 2023 saa 5:00 asubuhi, Balozi Baraka Luvanda akiambatana na Bw. Greyson Ishengoma, Afisa Ubalozi amewasilisha Hati za Utambulisho kwa Gavana Mkuu wa Jumuiya ya Madola ya Australia, Mheshimiwa David John Hurley. Hafla hiyo imefanyika katika ofisi za Gavana Mkuu, mjini Canberra na kuratibiwa na Balozi Ian McConville, Mkuu wa Itifaki na Bi. Fiona Holdsworth, Afisa Itifaki. 

Shughuli hiyo ilianza kwa Mheshimiwa Balozi Luvanda kusaini Kitabu cha wageni na baadaye kuelekea katika Ofisi ya Gavana Mkuu. Akikabidhi Hati za Utambulisho, Balozi Luvanda alifikisha salamu za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Mhe. Gavana Mkuu Hurley. 

Baada ya kukabidhi Hati za Utambulisho, Balozi Luvanda alipata fursa ya kufanya mazungumzo mafupi na Gavana Mkuu Hurley ambapo alimshukuru kutokana na nchi yake kuendelea kuisaidia Tanzania katika jitihada za kujiletea maendeleo ya kiuchumi kupitia elimu, kilimo na uwekezaji mkubwa katika sekta mbalimbali hususan, madini. 

Katika maelezo yake, Balozi Luvanda alitambua mchango mkubwa wa Australia kwenye sekta ya elimu kupitia Australia Award Scholarship Program, mpango ambao umewanufaisha vijana wengi wa kitanzania kusoma katika nyanja mbalimbali. Aidha, alieleza kuwa Serikali ya Tanzania itashukuru zaidi endapo Australia itaongeza nafasi za ufadhili kwa watanzania ikiwezekana hata katika ngazi ya astashahada na cheti. 

Kwa upande wake, Gavana Mkuu Hurley alieleza kuridhishwa kwake na sera za uwekezaji zinazotabirika chini ya Awamu ya Uongozi wa sasa ambazo zinawavutia wawekezaji wengi kutoka Australia. Aliongeza kuwa Serikali yake itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa pande zote mbili.

Vilevile, Gavana Mkuu Hurley alishukuru kwa salamu kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo aliomba salamu zake zifikishwe kwa Mhe. Rais na kumtakia afya njema.

Gavana Mkuu Hurley alihitimisha kwa kumkaribisha tena Balozi Luvanda na kumuahidi ushirikiano katika kipindi chote atakachokuwepo kwa manufaa ya nchi zote mbili. Baada ya mazungumzo hayo alimkaribisha Balozi Luvanda katika tukio la kupiga picha ya pamoja.