Tarehe 31 Januari, 2023 saa 7.40 mchana Balozi wa Tanzania nchini Japan ambaye pia anawakilisha nchini New Zealand, Mhe. Baraka Luvanda akiambatana na Bw. Hosea Chikolongo, Afisa Ubalozi na Bw. Stuart J. Batty, Balozi wa Heshima wa Tanzania nchini New Zealand, aliwasilisha Hati za Utambulisho kwa Gavana Jenerali na Amiri Jeshi Mkuu wa nchi hiyo Mheshimiwa Bi. Cindy Kiro. Wengine waliohudhuria shughuli hiyo iliyofanyika katika makazi ya Gavana (Government House) ni Mheshimiwa Dkt. Richard Davies – Mume wa Gavana, Wazee wawili wa kimila za kabila la Maori na Mkuu wa Itifaki Bw. Rod Harris.
Shughuli hiyo ilianza kwa Mheshimiwa Balozi Luvanda kusaini Kitabu cha wageni na sara maalumu kutoka kwa mmoja wa wazee wa kimila wa kabila la maori ambao ndiyo wazawa wa New Zealand.
Akitoa hotuba fupi kabla ya kukabidhi Hati, Balozi Luvanda alifikisha salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Gavana Jenerali na kusema kuwa mahusiano kati ya Tanzania na New Zealand yamejikita katika ushirikiano wa muda mrefu katika Jumuiya ya Madola na Umoja wa mataifa. Alimshukuru Gavana kutokana na nchi yake kuendelea kuisaidia Tanzania katika jitihada za kujiletea maendeleo ya kiuchumi kupitia kilimo, ufugaji, teknolojia na elimu katika fani mbalimbali na mafunzo ya muda mfupi, michezo na utamaduni.
Balozi Luvanda alieleza kuwa pamoja na umbali uliopo baina ya nchi hizi mbili, mahusiano baina ya watu wake yamedumishwa ambapo Watanzania wanajua uzuri wa nchi ya New Zealand na raia wa New Zealand wamekuwa wakiitembelea kwa wingi Tanzania kujionea vivutio vizuri vya utalii. Alihitimisha hotuba yake kwa kumkaribisha Gavana na familia yake kuitembelea Tanzania na kuomba ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake katika kipindi chote cha uwakilishi wake ili kudumisha na kukuza ushirikiano wa muda mrefu uliopo.
Aidha, baada ya kupokea Hati za Utambulisho, Mheshimiwa Cindy Kiro alimkaribisha Balozi Luvanda na kueleza kuwa amepokea salamu za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na kuwa nchi yake inatambua ushirikiano na uhusiano mzuri uliopo. Aliahidi kuendelea kutoa msaada katika sekta za uchumi ili kuinua maisha ya watanzania kupitia kilimo, ufugaji, Teknolojia na kutoa nafasi za masomo katika fani mbalimbali ambapo kwa sasa wapo Watanzania 42 wanaosoma nchini New Zealand na kwamba uwepo wa watanzania unasaidi katika kukuza na kubadilishana mila na utamaduni wa watu wake.
Vilevile, alituma salamu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na kumtakia afya njema pamoja na kutambua vuguvugu la madai ya Katiba mpya linaloendelea. Alihitimisha kwa kumkaribisha tena Balozi Luvanda na kumuahidi ushirikiano katika kipindi chote atakachokuwepo kwa manufaa ya nchi zote mbili. Baada ya kukamilika kwa shughuli hiyo walipiga picha za pamoja na kupata muda wa mazungumzo mafupi.






