Tarehe 16 Machi 2026, Balozi Anderson Mutatembwa alipokea ujumbe kutoka Kampuni ya Chuwa Industries ya Japan, inayojishughulisha na utengenezaji wa mitambo ya kuchoma taka (incinerators), hususan kwa uchakataji salama wa taka za hospitalini (medical waste). Majadiliano yalilenga kuanzisha ushirikiano na Tanzania katika kuwezesha upatikanaji na matumizi ya mitambo hiyo kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya afya na mazingira.
Ujumbe huo ulitoa wasilisho ukielezea shughuli na teknolojia za Kampuni ya Chuwa Industries, hususan katika utengenezaji na matumizi ya mitambo ya kuchoma taka za hospitalini, pamoja na uzoefu wao katika utekelezaji wa miradi mbalimbali duniani. Aidha, ilielezwa kuwa kampuni hiyo ina ushirikiano na baadhi ya nchi za Afrika, na tayari imeshiriki katika utekelezaji wa miradi ya kufunga mitambo ya kuchoma taka za hospitalini katika nchi kadhaa kwa kushirikiana na Serikali ya Japan kupitia Japan International Cooperation Agency pamoja na mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN).
Balozi Mutatembwa alitumia fursa ya mazungumzo hayo kuelezea fursa zilizopo nchini katika sekta ya usimamizi wa taka, ikiwemo uhitaji mkubwa wa udhibiti wa taka hatarishi za hospitalini, pamoja na umuhimu wa matumizi ya teknolojia salama na endelevu katika kulinda afya ya jamii na mazingira. Ilibainishwa kuwa mahitaji ya teknolojia hiyo yanaendelea kuongezeka sambamba na upanuzi wa huduma za afya na ongezeko la taka zinazozalishwa hospitalini na vituo vya afya.
Aidha, Balozi Mutatembwa alitoa shukrani kwa utayari wa kampuni hiyo kutoa mawasilisho ya kitaalamu au kupokea wataalam kutoka Tanzania kutembelea miradi yao inayoendelea katika nchi za Afrika, kwa ajili ya kujionea utekelezaji wa teknolojia hiyo kwa vitendo.
