Ubalozi unapenda kutoa taarifa kuwa Ujumbe wa wawekezaji 60 kutoka Japan, wanachama wa Shirikisho la Makampuni ya Japan kwa Maendeleo ya Miundombinu Afrika (Japan-Africa Infrastructure Development Association - JAIDA), utafanya ziara nchini Tanzania kuanzia tarehe 1 hadi 5 Oktoba 2024. Pamoja na mambo mengine, Ujumbe huo utashiriki kwenye Kongamano la Miundombinu la Tanzania na Japan (Tanzania - Japan Quality Infrastructure Dialogue) lililopangwa kufanyika tarehe 3 Oktoba 2024, jijini Dar es Salaam – Ukumbi wa Mikutano wa JNICC; na kuwa na mikutano ya ubia na taasisi mbalimbali za Tanzania kabla na baada ya Kongamano hilo.

Shirikisho la JAIDA ni muunganiko wa makampuni yapatayo, 191 yanayojishughulisha na ujenzi, uhandisi, ushauri elekezi, ukandarasi, viwanda, biashara na taasisi za fedha. Shirikisho hilo lilianzishwa mnamo mwezi Septemba 2016, mara baada ya kuhitimishwa kwa Kongamano la Miundombinu la Afrika na Japan (Africa-Japan Public Private Conference for High-Quality Infrastructure) pembezoni mwa Mkutano wa TICAD 6 mnamo mwezi Agosti 2016, jijini Nairobi. Shabaha kuu ya Shirikisho hilo ni kuziwezesha nchi za Afrika kuwa na miundombinu bora kwa kutumia ujuzi na teknolojia ya kijapani ikishirikisha ushirikiano wa ubia baina ya sekta za umma na binafsi kwa pande zote mbili, kwa kuandaa makongamano na ziara za ubia na nchi za Afrika.

Aidha, kwa upande wa Tanzania, Kongamano la Miundombinu la Japan na Tanzania huandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Japan kwa lengo la kukutanisha taasisi na makampuni ya miundombinu ya nchi hizo ambapo, mara ya mwisho lilifanyika mnamo mwaka 2018, kabla ya UVIKO - 19. Kongamano hilo huratibiwa na Wizara ya Ardhi, Miundombinu, Usafirishaji na Utalii ya Japan (MLIT) kwa ushirikiano wa Shirikisho la JAIDA; na kwa upande wa Tanzania, linaratibiwa na Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kwa ushirikiano wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Ujenzi, pamoja na wizara na taasisi zingine (umma na binafsi) zinazohusika na sekta za miundombinu ya ujenzi na uchukuzi za Tanzania Bara na Zanzibar.

Hamasa ya makampuni ya JAIDA kuitembelea Tanzania, imechochewa na uhamasishaji uliotokana na “Kampeni ya Kutangaza Fursa za Uwekezaji za Tanzania nchini Japan”, iliyofanyika kwa ushirikiano kati ya Ubalozi na Kituo cha Uwekezaji Tanzania ikiongozwa na Mheshimiwa Balozi Baraka Luvanda na Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Bw. Gilead Teri, mnamo mwezi Mei – Juni 2024 kwenye miji ya mikubwa ya kibiashara na viwanda Japan ya Tokyo, Osaka, Shizouka na Chiba.

Ujumbe wa wawekezaji hao nchini unatarajiwa kuongozwa na Bw. Ogasawara Kenichi, Naibu Waziri wa Ardhi, Miundombinu, Usafirishaji na Utalii ya Japan (MLIT) anayeshughulikia Miradi ya Kimataifa, atakayeambatana na Bw. Miyamoto Yoichi, Rais wa Shirikisho la JAIDA, pamoja na watendaji wa makampuni ya SHIMIZU CORPORATION; MITSUBISHI CORPORATION; TOYOTA TSUSHO CORPORATION; SUMITOMO CORPORATION; SUMITOMO MITSUI CONSTRUCTION CO., LTD; FUJITA CORPORATION; PADECO CO., LTD.; NIPPON STEEL CORPORATION; SAKAI HEAVY INDUSTRIES LTD.; JFE ENGINEERING CORPORATION; DELOITTE TOHMATSU CONSULTING LLC; YOKOGAWA BRIDGE CORP.; KATAHIRA & ENGINEERS INTERNATIONAL; NIPPON KOEI CO., LTD; NIPPON SIGNAL CO., LTD; QUNIE CORPORATION; ORIENTAL CONSULTANTS CO., LTD.; ORIENTAL CONSULTANTS GLOBAL; EBARA PUMPS EAST AFRICA; METAL ONE CORPORATION; n.k.

Ubalozi unatoa rai kwa sekta za umma na binafsi za Tanzania kutumia fursa ya Kongamano hilo na ziara ya wawekezaji hao nchini, katika kuibua au kuwezesha kuingia ushirikiano wa ubia na wawekezaji kutoka Japan, kupitia Ofisi za TIC au ZIPA zilizopo nchini.

Imetolewa na;
UBALOZI WA TANZANIA NCHINI JAPAN
TOKYO
26 SEPTEMBA 2024