Leo, tarehe 12 Novemba 2025, Ubalozi uliungana na Jumuiya ya Mabalozi na Wawakilishi wa Nchi mbalimbali waliopo Japan kushiriki katika Maonesho ya Kimataifa ya Mazingira na Teknolojia ya Kawasaki (Kawasaki International Eco-Fair 2025). Maonesho haya yalihusu ubunifu na teknolojia za kijani (green technologies) zinazolenga kupunguza uchafuzi wa mazingira, kuhamasisha matumizi ya nishati safi na kuimarisha uchumi wa mzunguko (circular economy).

Maonesho haya yameandaliwa kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Meya wa Jiji la Kawasaki na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO). Hafla ya ufunguzi ilihudhuriwa na viongozi wa Serikali ya Japan, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, sekta binafsi, na mabalozi wa nchi mbalimbali.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Meya wa Jiji la Kawasaki, Bw. Norihiko Fukuda, alisisitiza dhamira ya jiji hilo katika kupambana na uchafuzi wa mazingira kwa kutumia teknolojia bunifu. Alieleza kuwa, ingawa Kawasaki hapo awali ilikabiliwa na changamoto kubwa za viwandani kwa uchafuzi wa mazingira, sasa limekuwa mfano wa kimataifa kwa jiji lililofanikiwa kubadilisha changamoto hizo kuwa fursa kupitia maendeleo ya teknolojia safi na sera za kijani.

Aidha, Meya alibainisha kuwa maonesho ya mwaka huu yamevutia zaidi ya kampuni 120, ambapo takribani 80 kati ya hizo zinatoka ndani ya Jiji la Kawasaki. Kampuni hizo ziliwasilisha teknolojia na bidhaa mbalimbali zinazohusiana na nishati mbadala, ufanisi wa rasilimali, usimamizi wa taka, na ubunifu wa viwanda visivyochafua mazingira.

Kwa upande wa Ubalozi, ushiriki katika maonesho haya ulilenga kujifunza mbinu bora za Japan katika kukuza teknolojia rafiki kwa mazingira na kutafuta fursa za ushirikiano kati ya Tanzania na Japan katika maeneo ya nishati safi, uchumi wa mzunguko (circular economy), na maendeleo ya viwanda endelevu. Ushiriki huo ni muhimu zaidi kwa kuzingatia kuwa Tanzania imesaini Makubaliano ya Ushirikiano (MOC) na Serikali ya Japan mnamo mwezi Mei 2025, kuhusu utekelezaji wa “Carbon Credit Mechanism”, hatua inayolenga kuimarisha ushirikiano wa Japan na Tanzania katika kupunguza hewa ukaa na kukuza uchumi wa kijani kupitia miradi ya pamoja ya mazingira.

Ubalozi umepongeza juhudi za Jiji la Kawasaki na UNIDO kwa kuandaa jukwaa hili muhimu linalochochea ubadilishanaji wa maarifa na ushirikiano wa kimataifa katika kulinda mazingira na kukuza maendeleo endelevu.