Tarehe 6 Februari 2026, Balozi Anderson Mutatembwa, alitembelea Makao Makuu ya JGC Corporation jijini Yokohama na kuwa na mazungumzo na Makamu wa Rais wa Kampuni hiyo, Bw. Koji Sakurai. Mazungumzo hayo yalijikita katika tathmini ya utekelezaji wa Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) yaliyosainiwa kati ya Wizara ya Nishati na Kampuni ya JGC, mwezi Mei 2025, wakati wa Maonesho ya EXPO OSAKA 2025, Jijini Osaka; pamoja na hatua zinazoendelea kuelekea utekelezaji wa Mradi wa LNG nchini Tanzania.
Katika mazungumzo hayo, Balozi Mutatembwa alieleza dhamira ya Serikali kuendelea kushirikiana na makampuni ya Kijapani ikiwemo JGC, katika nyanja za uhamishaji wa teknolojia, kujenga uwezo wa kitaalamu na kuimarisha ushiriki wa Watanzania katika mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya gesi asilia. Pia, aliomba kuangaliwa uwezekano wa kuanzisha programu ya kushikiza (secondment/attachment program) kwa maafisa na wataalamu wa Tanzania ili waweze kupata uzoefu wa vitendo katika miradi inayotekelezwa na JGC katika maeneo mbalimbali duniani, hususan katika uhandisi, usimamizi wa miradi, uendeshaji na matengenezo ya mitambo ya LNG.
Aidha, Mheshimiwa Balozi alipata fursa ya kufunga rasmi mafunzo ya wataalamu wa nishati kutoka Tanzania yaliyofanyika kwa muda wa wiki moja katika Makao Makuu ya JGC. Mafunzo hayo yalijikita katika sekta ya LNG, ikiwemo: misingi ya gesi asilia na mchakato wa uongoshaji (liquefaction), miundombinu ya uzalishaji na uchakataji wa gesi (upstream processing facilities), teknolojia za mitambo ya LNG, usimamizi na uratibu wa miradi mikubwa (project management and scheduling), tathmini ya kiuchumi ya miradi ya LNG, pamoja na mbinu za kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa (low carbon solutions).
Vilevile, kupitia hotuba yake ya kufunga mafunzo hayo, alitoa shukrani za Tanzania kwa JGC na JICA kwa mchango wao katika kujenga uwezo wa wataalamu wa Tanzania, na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano huo kwa kuzingatia mahitaji ya kimkakati ya nchi katika utekelezaji wa Mradi wa LNG.




