Hivi karibuni, Ubalozi kwa kushirikiana na Kampuni ya GOSHENI SAFARIS ya Tanzania (Mtoa Huduma Bora Namba Moja wa Kitalii Afrika 2024 - Tuzo za Usafiri za Dunia 2024) ulifanikisha ziara ya kitalii na kimafunzo (Familiarization Trip - Fam Trip) kwa kampuni sita (6) kubwa za utalii za Japan. Kampuni hizo za Japan ni DOSOSHIN INC., SALONGO INC., JST CORPORATION, TEESTYLE, GLAGE INC., na LUMIÈRE DOUCE CO. LTD.

Makampuni hayo pia yalipata nafasi ya kushiriki katika Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Swahili (S!TE 2024) yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, tarehe 11 - 13 Oktoba 2024; na kuendelea na Fam Trip iliyoandaliwa na GOSHENI SAFARIS kwa kutembelea vivutio vya utalii vya Tarangire, Manyara, Ngorongoro, Serengeti, Arusha na Zanzibar.

Kwa upande wake, Mheshimiwa Balozi Baraka Luvanda alipata wasaa wa kuwakaribisha Ubalozini, leo tarehe 1 Novemba 2024, wawakilishi wa makampuni hayo kwa lengo la kupokea mrejesho wa ziara walioifanya nchini.

Balozi Luvanda alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa makampuni hayo kuendelea kuichagua Tanzania kama kivutio namba moja katika shughuli zao za kupeleka watalii sehemu mbalimbali duniani. Aliwaahidi ushirikiano wa Ubalozi na wa Tanzania kwa ujumla, katika shughuli zao na kuitangaza Tanzania kama sehemu sahihi ya utalii kwa wajapani.