Ubalozi wa Tanzania nchini Japan umekuwa ukipokea malalamiko yayohusu kutapeliwa magari toka kwa watanzania wanaoagiza magari yaliyotumika nchini Japan.  Malalamiko hayo hupokelewa moja kwa moja kutoka wa watanzania hao kwa njia ya barua pepe na kupitia Wizarani. Malalamiko hayo ni pamoja na yafuatayo:

(i)         Mtu kutuma fedha kwa kampuni baada ya kuona gari kwenye mtandao na kuanzisha mazungumzo na kukubaliana malipo na baadaye kutotumiwa gari alilolipia na mawasiliano na wahusika kukatika.

(ii)        Mtu kuagiza gari kwa bei fulani na baada ya kutuma fedha hudaiwa malipo ya ziada ili aweze kutumiwa gari kinyume na makubaliano ya awali.

(iii)       Mtu kuagiza gari na baada ya malipo hutumiwa gari hiyo bila nyaraka zinazotakiwa ili aweze kulitoa Bandarini na anapowasiliana na wahusika humtaka atume malipo ya ziada ili atumiwe nyaraka.

(iv)       Mtu kutumiwa gari tofauti na aliloliagiza (chakavu tofauti na aliloliona kwenye mtandao). 

(v)        Kwa wanaofanya biashara ya magari, hutumiwa baadhi ya magari waliyoagiza na kutapeliwa mengine.

Ubalozi umekuwa ukifanyia kazi malalamiko yao ambayo kwa kiasi kikubwa hushindwa kuwasaidia kupata magari wanayodai baada ya kuyalipia au kurejeshewa fedha walizotuma kutokana na sababu zifuatazo:

(i)         Baada ya Balozi nyingi hususan, za nchi za Afrika kupata malalamiko na namna hiyo, kuliwahi kufanyika  kikao kati ya Balozi hizo na Wizara ya Mambo ya Nje ya Japan (MOFA) ambao walisema kuwa inakuwa vigumu kwa Serikali ya Japan kufanyia kazi malalamiko hayo kutokana na kutokuwepo kwa mikataba ya kisheria bali makubaliano binafsi kwa njia ya mtandao.  Majibu hayo yamekuwa yakitolewa mara kwa mara kila wanapopewa taarifa za utapeli huo. 

(ii)        Kampuni nyingi zinazolalamikiwa ni za matapeli na hazina anuani kamili zinazotambulika tofauti na zinavyosomeka katika mitandao hali inayosababisha ugumu katika kuwatafuta walipo. 

(iii)       Mawasiliano yanayofanywa kati ya watanzania wanaoagiza magari na makampuni ni kwa njia ya whatsap ambapo namba za simu nyingi zinazotumika ni za nje ya Japan na hivyo kuwa vigumu kuwapata matapeli hao kwa njia ya simu za kawaida.

(iv)       Makampuni machache yanayopatikana na kufikishiwa malalamiko hayo hukiri kupokea fedha na kusingizia kutopata nafai katika meli ili kusafirisha magari ya wateja wao na kuahidi kutuma magari hayo mara watakapopata nafasi katika meli sababu ambazo si za kweli.  Pia yapo ambayo huahidi kurudisha fedha za wateja walioagiza magari baada ya kukwama kuwapelekea magari waliyoagiza.  Hata hivyo kumekuwa na ugumu wa kufanya hivyo.

(v)        Ubalozi umekuwa ukiwashauri watanzania wanaoulizia uhalali wa kampuni wanazotaka kuagiza magari kabla ya kuagiza na wamekuwa wakipokea magari wanayoyahitaji bila kuwa na usumbufu wowote.

Tunaendelea kushauri watu wanaoagiza magari kuingia katika mtandao wa Chama cha Wasafirishaji wa Magari Yaliyotumika cha Japan (Japan Used Motor Vehicle Exporters Association – JUMVEA) ambacho ni chama kinachofanya vizuri katika uhakiki wa kampuni zinazoagiza magari kwa uhakika (www.jumvea.or.jp) ili kuhakiki kampuni wanazotaka kuagiza magari kabla ya kuagiza magari hayo kuepuka kutapeliwa.  Aidha, tunashauri watumie makampuni ya kijapan ya uuzaji magari yaliyosajiliwa na yenye ofisi Tanzania kwa kuwa wanao uwezo wa kuwachukulia hatua za kisheria wanaposhindwa kuwapatia magari waliyoagiza.  Kwa kufanya hivyo, tunaamini tutaepusha kwa kiasi kikubwa vitendo vya kitapeli ambavyo vimeendelea kuongezeka siku hadi siku. KWA PAMOJA TUNAWEZA KUZUIA UTAPELI HUU NA HASARA INAYOAMBATANA NA VITENDO HIVYO.

 

MEI 2022                                    UBALOZI WA TANZANIA, TOKYO - JAPAN