Tarehe 18 Disemba 2025, Balozi Anderson Mutatembwa aliupokea Ubalozini, Ujumbe wa wataalamu saba (07) kutoka Tanzania unaojumuisha wawakilishi kutoka Wizara ya Fedha; Wizara ya Fedha na Mipango – Zanzibar; Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali; na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Ujumbe huo uliongozwa na Dr. Remidius Ruhinduka, Kamishna wa Uchambuzi wa Sera, Wizara ya Fedha ya Tanzania.
Ujumbe huo unashiriki majadiliano ya duru ya pili ya Mkataba wa Kuondoa Utozaji Kodi Mara Mbili na Kuzuia Uepaji na Ukwepaji Kodi (Double Taxation Agreement – DTA) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Japan, yanayofanyika kuanzia tarehe 16 hadi 19 Disemba 2025, katika Makao Makuu ya Wizara ya Fedha ya Japan, jijini Tokyo.
Ujumbe ulitoa taarifa kwa Balozi Mutatembwa kuhusu mwenendo wa majadiliano, mafanikio yaliyopatikana hadi wakati huo, pamoja na baadhi ya vifungu vinavyohitaji majadiliano zaidi katika duru zijazo.
Balozi Mutatembwa kwa upande wake aliipongeza timu ya wataalamu kwa kazi nzuri iliyofanyika hadi hatua hiyo, na kuwasisitiza kuendelea kujadiliana kwa weledi na umakini huku wakilinda maslahi mapana ya Taifa katika kufanikisha ukamilikaji wa Mkataba huo. Pia, aliwaahidi ushirikiano wa Ubalozi kadri itakavyohitajika katika kufanikisha majadiliano hayo.



