Tarehe 16 Februari 2026, Mheshimiwa Balozi Anderson Mutatembwa alipokea ugeni wa Bw. Shigeki Komatsubara, Mkurugenzi Mkaazi wa United Nations Development Programme (UNDP) nchini Tanzania.
Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano wa maendeleo kati ya Tanzania, UNDP na Japan, hususan katika maeneo ya maendeleo jumuishi, uchumi wa kijani, ubunifu wa maendeleo (innovation), pamoja na miradi ya kujenga ustahimilivu wa kiuchumi na kijamii. Aidha, pande zote zilijadili fursa za kuendeleza ushirikiano wa kimkakati kati ya UNDP na wadau wa maendeleo wa Japan, ikiwemo Japan International Cooperation Agency, katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini Tanzania.
Katika mazungumzo hayo, Bw. Komatsubara alieleza dhamira ya UNDP kuendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kusaidia utekelezaji wa vipaumbele vya maendeleo ya Taifa, ikiwemo kuimarisha sekta ya kilimo, uchumi wa buluu, nishati jadidifu, pamoja na mifumo ya kidigitali kwa maendeleo endelevu. Alisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano wa pande tatu (triangular cooperation) kati ya Tanzania, UNDP na Japan ili kuongeza ufanisi wa miradi ya maendeleo na uhamishaji wa teknolojia na utaalamu.
Kwa upande wake, Mheshimiwa Balozi Mutatembwa alishukuru mchango endelevu wa UNDP katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini Tanzania, na kusisitiza kuwa ushirikiano kati ya UNDP na taasisi za Japan, hususan JICA, umeendelea kuwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ujenzi wa uwezo wa taasisi na kuimarisha ubunifu wa maendeleo.
Aidha, alieleza utayari wa Ubalozi kuendelea kuratibu na kuimarisha ushirikiano kati ya UNDP, Serikali ya Japan na taasisi zake za maendeleo ili kuibua na kutekeleza miradi yenye tija zaidi kwa Tanzania, sambamba na kuhimiza kuongezwa kwa miradi ya pamoja inayochangia ajenda ya maendeleo endelevu na malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa.



