Tarehe 30 Disemba 2024, Balozi Baraka Luvanda alishiriki katika Mkutano wa Mwaka 2024 wa Umoja wa Wanafunzi wa Kitanzania nchini Japan (TSJ) uliofanyika katika Ubalozi, Tokyo. Mkutano huo ulijumuisha baadhi ya Viongozi waliomaliza muda wao, Viongozi wapya na wajumbe wa Umoja huo. 
Katika hotuba yake, Makamu Mwenyekiti wa Umoja huo Bi. Eva Sarakikya alimshukuru Balozi Luvanda kwa kukubali kuwa mwenyeji wa mkutano huo na kukubali mwaliko wa kushiriki katika mkutano wa mwaka, ukiwa ni mkutano wa nne tangu Umoja huo uanzishwe rasmi mwaka 2021. Pia alimshukuru Balozi kwa kuwa mlezi wa Umoja huo kwa kipindi hicho chote, kazi ambayo ameifanya vizuri na kupelekea TSJ kupata mafanikio makubwa chini ya ulezi wake. 
Aidha, Bi. Sarakikya aliwasilisha taarifa ya utendaji ya TSJ ya mwaka 2024 ambayo ilitaja mafanikio na changamoto ambazo Umoja umepitia. Baadhi ya mafanikio ambayo TSJ iliyafikia ni pamoja na: kuongeza idadi ya wanachama hai na kufanya idadi  ya sasa kuwa 86; kuendeleza mpango wa kusambaza na kuuza vyakula vya kitanzania kwa wanachama wake jambo ambalo limeongeza kipato cha umoja; na kuendesha mafunzo kuhusu fursa za masomo nchini Japan, hususan kupitia program ya MEXT. Hata hivyo, Bi. Sarakikya alitaja baadhi ya changamoto zikiwemo: kusuasua kwa ulipaji wa ada wa uanachama unaopolekea uhaba wa kifedha katika uendeshaji wa Umoja, na kusuasua kwa wanafunzi kujiunga na Umoja huu kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kutokuwa na taarifa sahihi juu ya manufaa ya kuwa mwanachama.  
Kufuatia changamoto hizo, Bi. Sarakikya aliainisha mikakati iliyopo ambayo ni pamoja na: kuimarisha mifumo ya mawasiliano ili kuhakikisha kila mwanafunzi wa kitanzania anayesoma nchini Japan anakuwa sehemu ya TSJ; kuendelea kuboresha mpango wa ukusanyaji ada; kupanua wigo wa matukio ya kijamii na kielimu kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali; na Kukuza ushirikiano wa karibu zaidi kati ya TSJ na Ubalozi.

Akihitimisha hotuba yake, Bi. Sarakikya aliwatambulisha Viongozi wapya wa TSJ waliochaguliwa tarehe 28 Disemba, 2024 ambao wataongoza kwa muda wa mwaka mmoja (1). Viongozi hao ni: Bw. Kinuma Shabani Ndaki - Mwenyekiti; Bw. Anicet Majambele Lugendo - Katibu; Bw. Marco Abdon Marco - Naibu Katibu; na Bw. Daniel Innocent John - Mweka Hazina
Alishukuru kwa ushirikiano mkubwa ambao Balozi na Maafisa wake wamekuwa wakiwapatia viongozi wanaomaliza muda wao na kuomba ushirikiano uendelee kwa viongozi wapya ili kuifanya TSJ iwe imara na yenye mafanikio zaidi. 
Kwa upande wake, Balozi Luvanda aliwashukuru Uongozi wa TSJ kwa kumwalika kila mwaka kushiriki katika Mikutano yao ya Mwaka ukiwemo huu wa sasa. Pia, aliwapongeza viongozi waliohitimisha awamu ya uongozi kwa mafanikio makubwa na kuwapongeza Viongozi wapya kwa kuchaguliwa akiwatia shime kuendeleza umoja huu na kuuimarisha zaidi. 
Balozi Luvanda aliendelea kwa kueleza kufarijika kwake kwa mafanikio ya umoja huu ndani ya kipindi cha mwaka mmoja na kwamba ushirikiano uliojengwa baina ya wanachama sio tu wa kielimu bali pia wa kijamii. Amewapongeza pia Viongozi na wanaumoja huo kwa kutumia fursa mbalimbali kuitangaza nchi yetu kwa kushiriki katika matukio mbalimbali ambako wamekuwa wakipeperusha vema bendera ya Tanzania nchini Japan. 
Balozi Luvanda pia aliipongeza TSJ kwa kazi nzuri ya malezi kwa wanajumuiya wapya kila wanapoingia nchini Japan. Alirejea kutoa rai kwa wana TSJ kama ambavyo amekuwa akifanya kila mara anapokutana nao kuwataka kuendelea kuwa wageni wazuri nchini Japan kwa kuendelea kutii sheria za wenyeji wetu bila shuruti ambapo kwa kufanya hivyo watakuwa wamedumisha sifa nzuri ya Tanzania.
Akihitimisha, Balozi Luvanda aliwahakikishia wana TSJ kuwa milango ya Ubalozi iko wazi wakati wote kwa aina yoyote ya huduma na kwamba Ubalozi utaendelea kushirikiana na umoja huo bega kwa bega katika kutekeleza mipango ya umoja huo; kuendeleza; na kubuni mipango mipya kwa pamoja na kushirikiana kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazojitokeza. Mwishoni, Balozi Luvanda aliwakabidhi vyeti Viongozi waliomaliza muda wao wa Uongozi.