Tarehe 19 Machi 2023, Mhe. Balozi Baraka Luvanda alikutana na kufanya mazungumzo na Jumuiya ya Watanzania (Diaspora) walioko nchini Japan ijulikanayo, Tanzanite Society, kwenye Makazi ya Balozi, jijini Tokyo. Mkutano huo ulikuwa wa kwanza kufanyika kwa mwaka 2023, na ulilenga pamoja na mambo mengine, kujuliana hali; kupokea mipango mikakati iliyowekwa na Jumuiya ya Watanzania; na kufanya uchaguzi wa kupata viongozi wa Jumuiya hiyo. 

Akiwasilisha taarifa ya mwenendo wa Jumuiya ya Tanzanite kwa muda wa kipindi cha miaka miwili 2021/2022 – 2022/23, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Bw. Frank Semaganga alielezea maeneo ambayo yalitiliwa maanani katika ungozi huo ikiwemo, kurejesha imani ya wanachama kwa wanajumuiya hiyo, kuongeza uwazi kwenye masuala ya fedha ya Jumuiya, kuimarisha mshikamano na maelewano baina ya Wanajumuiya, kuongeza mwelekeo wa idadi ya wanachama hai pamoja na mfuko wa ada za uanachama, kuendelea na maboresho ya katiba ya Jumuiya kuendana na mabadiliko ya nyakati na kuitangaza Jumuiya yetu nyumbani ili kuongeza ujulikanaji wa Jumuiya yetu kwa Taasisi na wadau wa Diaspora walioko Tanzania. 

Bw. Semaganga alielezea namna Jumuiya hiyo ilivyoshirikiana kwa pamoja katika kupokea ugeni wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, alipotembelea Japan mwezi Septemba 2022 ambapo alimwakilisha Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye mazishi ya aliyekuwa Waziri Mkuu Mstaafu wa Japan, Bw. Shinzo ABE.  

Aidha, Bw. Semaganga alieleza kuwa katika awamu ya uongozi wake, Jumuiya ya Tanzanite imeshuhudia kuanzishwa kwa Umoja wa Wanafunzi Watanzania nchini Japan ijulikanayo, the Tanzania Students Association in Japan (TSJ), mnamo mwezi Disemba 2021. Vilevile, alielezea matumaini ya Jumuiya ni kuwa Umoja wa TSJ utatumika kama chombo cha kuwaleta pamoja na kuwaunganisha jamii ya wanafunzi watanzania wanaosoma nchini Japan na pia kuwa kiunganishi baina ya Tanzanite na TSJ.

Kwa upande wake, Balozi Luvanda alishukuru kwa mwitikio mkubwa wa Diaspora hao kutoka pande zote za Japan kwa kujitokeza kwa wingi na kujumuika pamoja katika siku hiyo muhimu iliyoandaliwa kwa ajili yao. Aliupongeza uongozi kwa kazi kubwa inayofanya ya kuwaunganisha Watanzania wote walioko nchini Japan, na kueleza kuwa hiyo haikuwa kazi rahisi hususan, kwa kuzingatia uwepo wa changamoto nyingi za kuiunganisha jumuiya hiyo kutokana na mitazamo binafsi iliyokuwepo. 

Balozi Luvanda alielezea faraja yake ya kuona kuwa Uongozi huo umeanza kurejesha imani ya wanachama wa jumuiya hiyo kwa kuongeza uwazi kwenye masuala ya fecha, kuimarisha mshikamano na maelewano ya wanajumuiya, kuongeza idadi ya wanachama hai, kuboresha Katiba ya Jumuiya na kuitangaza Jumuiya ndani na nje ya Japan. 

Balozi Luvanda aliwakumbusha Watanzania hao wajibu wao wa kutii sheria bila shuruti na taratibu za nchi mwenyeji (Japan), kwani kutokutii sheria kunaweza kuiletea sifa mbaya sio tu jamii ya Watanzania waishio Japan bali kwa Taifa la Tanzania, kwa ujumla. Aliwakumbusha pia kudumisha uzalendo kwa nchi yao Tanzania na kuitangaza vizuri Tanzania kwa kuwavutia watalii, wafanyabiashara na wawekezaji wa Kijapani kuja nchini. 

Vilevile, Balozi Luvanda aliwapongeza kwa kujenga ushirikiano wa kusaidia na katika masuala mengi ya kiuchumi, kindugu na kijamii. Alitolea mfano mashindano maarufu ya mpira wa miguu kupitia Timu ya Mpira ya Miguu ya Diaspora ya Tanzania ijulikanayo “The Kilimanjaro FC” ambayo imekuwa ikifanya vizuri katika kuitangaza nchi yetu na kupeperusha vema bendera ya Tanzania nchini Japan kupitia michezo. 

Mkutano huo ulishuhudia pia tukio la uchaguzi wa viongozi wa Jumuiya ya Tanzanite watakaohudumu kwa kipindi cha miaka miwili ijayo, 2023/2024 – 2024/2025. Uchaguzi huo uliendeshwa kwa ushirikiano na Maafisa Ubalozi, uliwapa viongozi wapya wafuatao: Mwenyekiti wa Jumuiya, Bw. Frank Semaganga (amechaguliwa tena); Makamu Mwenyekiti, Bi. Beatrice Narita (nafasi mpya); Katibu Mkuu, Bw. Ramadhan Kingwande (nafasi mpya); Katibu Msaidizi, Dr. Balimponya Elias (nafasi mpya); Mweka Hazina, Bi. Zawadi Mwimbage (nafasi mpya); Mweka Hazina Msaidizi, Bw. Willy Fred Felix (nafasi mpya); na Katibu Uenezi, Bw. Theophily Mfunami Pembe (amechaguliwa tena). 

Viongozi hao wapya waliochaguliwa walipewa maazimio ya vipaumbele vya Jumuiya ikiwemo, kuharakisha maboresho ya rasimu ya Katiba ya Jumuiya na kuipitisha kuwa Katiba kamili; kuhimiza wanajumuiya kulipa ada za mwaka kwa wakati ili kupata wanachama hai wengi zaidi; kutengeneza kalenda ya mwaka ya matukio muhimu ya Jumuiya; kuongeza wigo wa ushirikiano baina ya Tanzanite na TSJ; kuandaa mikakati ya muda mrefu na mfupi kwa ajili ya shughuli za uwekezeji na utoaji misaada Tanzania; kuimarisha mshikamano baina ya wanajumuiya; na kuongeza ushiriki wa wanajumuiya hao kwenye mambo mbalimbali yahusuyo Jumuiya. 

Mkutano huo ulihitimishwa kwa tukio la Timu ya Mpira wa Miguu ya Kilimanjaro FC kukabidhi Kombe la Ushindi kwa Balozi Luvanda, walioupata wakati wa michezo ya “The Futsal Friendly Match Cup” kwa kushika nafasi ya pili. Michezo hiyo ilifanyika mwezi Julai 2022; na kushirikisha timu za mpira wa miguu za Diaspora, zipatazo nane (8).