Tarehe 6 Februari 2026, Balozi Anderson Mutatembwa, alifanya mazungumzo na Meya wa Jiji la Yokohama, Mheshimiwa Takeharu Yamanaka (Ph.D), yaliyolenga kuimarisha ushirikiano kati ya Jiji la Yokohama na Tanzania kupitia Jiji la Dar es Salaam. Miongoni mwa yaliyojadiliwa ni maandalizi ya Hati ya Ushirikiano (MoU), pamoja na kubainisha maeneo ya kipaumbele yatakayotekelezwa kwa manufaa ya pande zote mbili. 

Katika mazungumzo hayo, Meya Yamanaka alibainisha utayari wa Jiji la Yokohama kuendeleza ushirikiano na Jiji la Dar es Salaam, kufuatia mazungumzo ya awali yaliyofanyika wakati wa Mkutano wa TICAD 9, ambapo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, alionesha nia ya kuanzisha ushirikiano wa majiji (city-to-city relations). Meya huyo alishukuru kwa mawasiliano yanayoendelea na Ubalozi kuhusu ukamilishwaji wa rasimu ya MoU na kwamba wanatarajia kuendeleza mawasiliano na majadiliano hadi kufikia hatua ya kusaini makubaliano rasmi.

Kwa upande wake, Balozi Mutatembwa alimshukuru Meya Yamanaka kwa dhamira yao ya kuanzisha ushirikiano na Tanzania kupitia Jiji la Dar es Salaam na kuthibitisha kuwa rasimu ya MoU kutoka Jiji la Dar es Salaam iko katika hatua za mwisho za mapitio ya ndani na itawasilishwa rasmi mara tu taratibu za mapitio nchini, zitakapokamilika. Alibainisha kuwa ushirikiano kati ya majiji hayo mawili utawezesha kubadilishana uzoefu na utaalamu katika maeneo ya usimamizi wa taka na uchumi wa mzunguko (circular economy), uboreshaji wa huduma za kijamii, pamoja na kukuza biashara, uwekezaji na utalii. Aidha, alisisitiza kuwa ushirikiano huo utatoa fursa za mafunzo na ujenzi wa uwezo kwa watumishi wa majiji husika, kubadilishana ziara za wataalamu na wanafunzi, na kuanzisha majukwaa ya sekta binafsi kwa ajili ya kuhamasisha ubia na uwekezaji kati ya pande hizo mbili.

Aliongeza kuwa hatua hiyo itaongeza mshikamano na uelewano wa wananchi wa majiji hayo mawili, na hivyo kuimarisha zaidi uhusiano wa kidiplomasia na kirafiki kati ya Tanzania na Japan uliojengeka kwa takribani miongo sita iliyopita.

  • Balozi Anderson Mutatembwa, kwenye picha ya pamoja na Meya wa Jiji la Yokohama, Mheshimiwa Takeharu Yamanaka (Ph.D), mara baada ya mazungumzo yaliyolenga kuimarisha ushirikiano kati ya Jiji la Yokohama na Tanzania kupitia Jiji la Dar es Salaam.Balozi Anderson Mutatembwa, kwenye picha ya pamoja na Meya wa Jiji la Yokohama, Mheshimiwa Takeharu Yamanaka (Ph.D), mara baada ya mazungumzo yaliyolenga kuimarisha ushirikiano kati ya Jiji la Yokohama na Tanzania kupitia Jiji la Dar es Salaam.