Leo, tarehe 1 Oktoba 2024, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri, akiwa na Balozi Baraka Luvanda, Balozi wa Tanzania nchini Japan; amezungumza na waandishi wa habari na kutoa ripoti kuhusu hali ya Uwekezaji nchini kwa kipindi cha Aprili mpaka Juni 2024. Katika mkutano huo, wamesisitiza mambo mawili muhimu: ongezeko la miradi ya uwekezaji nchini pamoja na kongamano la miundombinu kati ya Tanzania na Japan linalotarajiwa kufanyika tarehe 3 Oktoba 2024 katika ukumbi wa JINCC.

Teri alifafanua kuwa, katika kipindi cha Aprili hadi Juni 2024, TIC imeweza kusajili miradi 198 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.6  ambayo inatarajia kuleta ajira takriban 96,000. Hii ni hatua kubwa ikilinganishwa na miradi 129 iliyosajiliwa kipindi kama hicho yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1 na ajira tarajiwa 14631, Ongezeko hilo ni la asilimia 53.4 kwa upande wa usajili wa miradi na asilimia 60.72 lenye ukuwaji wa thamani za miradi wakati huo huo kukiwa na ongozeko kubwa la asilimia 558.04 katika ongezeko la ajira zinazotarajiwa.

Teri aliongeza kuwa kuna mafanikio makubwa ya kipindi cha robo mwaka ya kwanza kuanzia julai mpaka septemba 2024 ambapo jumla ya miradi iliyisajiliwa 259 ukilinganisha na miradi 137 iliyosajiliwa katika kipindi kama hicho.

Alisisitiza kwamba ukuaji huu unatokana mafanikio makubwa yaliyopatika kutokana na uboreshaji wa mazingira na biashara  na uwekezaji yaliyofanywa na serikali ya awamu ya sita.

Kwa upande wake, Balozi Baraka Luvanda aliwataka Watanzania kuchangamkia fursa hii ya kongamano, akisisitiza umuhimu wa kubadilishana uzoefu na kushirikiana katika kukuza na kuboresha miundombinu nchini. Alisema, "Tukio hili ni muhimu kwa ajili ya kujenga uchumi wa nchi na kuimarisha sekta zinazohusiana na miundombinu."

Kongamano hili  linatarajiwa kuwa na ushiriki wa  makampuni 60 kutoka Japan zitakutana na wawekezaji wa Tanzania.  Matarajio ya  mkutano huo ni kujadili masuala yanayohusiana na maendeleo ya miundombinu, na kutoa nafasi kwa kampuni za Japan na Tanzania kushirikiana katika miradi mbalimbali, ambayo itachangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa taifa. 

 

IMETOLEWA NA KITUO CHA UWEKEZAJI TANZANIA (TIC)

TAREHE 01 OKTOBA 2024