Tarehe 9 Juni 2023, wakati wa uzinduzi wa uuzaji wa kahawa ya Tanzania katika migahawa ya Tully's Coffee iliyoko Japan, Mheshimiwa Balozi Baraka Luvanda alifanya mahojiano maalum na Shirika la Utangazaji la Japan - NHK, Idhaa ya Kiswahili kuelezea mwenendo wa soko la kahawa ya Tanzania nchini Japan.
Maongezi hayo yalijikita katika kuelezea jitihada za Serikali ya Tanzania katika kuendeleza sekta ya kilimo nchini; pamoja na zile za Ubalozi za kutafuta masoko ya bidhaa za Tanzania hususan, bidhaa za kilimo kama vile, kahawa ambayo Kampuni ya Tully's imeanza kuiuza katika migahawa yao yote nchini Japan.
Ifuatayo ni dondoo ya maongezi ya Mhe. Balozi Baraka Luvanda na Shirika la NHK Japan, Idhaa ya Kiswahili:
DONDOO ZA MAONGEZI NA NHK
Jambo! Konichiwa!
1. Jina langu ni Baraka Luvanda, Balozi wa Tanzania nchini Japan, nikiwa na dhamana ya kuiwakilisha pia nchi yetu katika nchi za Australia, New Zealand na Papua New Guinea.
2. Leo tumekusanyika hapa katika mojawapo ya makampuni makubwa nchini Japan yanayojishughulisha na biashara ya chakula Japan na barani Asia, kwa ujumla. Kusanyiko hili ni mahsusi kwa ajili ya kushuhudia kwa furaha na bashasha kubwa hafala ya uonjaji wa kahawa ya Tanzania, chapa ya GDM inayozalishwa huko Mbozi mkoani Mbeya, Tanzania. Nitumie nafasi hii kuipongeza kwa dhati Kampuni ya GDM ambayo ni kampuni ya kitanzania kwa mafanikio haya makubwa.
3. Kahawa hii imezinduliwa rasmi jusi tarehe 7 Juni 2023 katika migahawa mikubwa na maarufu ya Japan ambayo inapatikana katika viunga vyote vya Japan.
4. Kuzinduliwa kwa kahawa ya GDM hapa Japan kunapandisha zaidi uhakika wa soko la kahawa ya Tanzania nchini Japan ambayo imejizoelea umaarufu mkubwa kwa ubora na radha ya aina yake na kupewa jina la kibiashara la Tanzania Kilimanjaro Coffee. Kahawa ya Tanzania inayouzwa nchini Japan ni kutoka mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Kagera, Mara, Tanga, Morogoro, Njombe, Iringa, Katavi, Rukwa, Ruvuma, Kigoma, Songwe na Mbeya.
5. Hivyo, napenda kuchukua nafasi hii, kutoa rai kwa watanzania wote hususan, wakulima wa zao la kahawa, watayarishaji, wasafirishaji na wafanyabiashara wa zao hili kuchangamkia fursa ya soko hili la Japan ambalo linakuwa siku hadi siku.
6. Kwa mujibu wa takwimu kutoka Bodi ya Kahawa Tanzania Japan ni nchi ya kwanza inayonunua kahawa ya Tanzania kwa wingi ambapo, kwa mwaka Tanzania inauza kahawa nchini Japan, wastani wa asilimia 33 ya kahawa inayolimwa nchini, Kiwango hicho ni sawa na wastani wa tani 15,000 ya kahawa ya Tanzania inayouzwa Japan, ikilinganishwa na matumizi na uhitaji wa Japan wa wastani wa tani laki nne na elfu hamsini na tatu za kahawa kwa mwaka (tani 453,000). Hivyo, ni dhahiri kuwa soko la kahawa hapa nchini Japan, bado ni kubwa na hiyo ni fursa adhimu kwa watanzania wenzangu.
7. Napenda kutoa wito kwa watanzania wenzangu kuzingatia ubora wa viwango kwa mazao tunayolima nchini kwani nchi nyingi tunakouza bidhaa zetu hususan, hapa Japan wanazingatia sana viwango. Hivyo, ili kulikamata soko hili la Japan ipasavyo, inatupasa kwenda sambamba na mahitaji ya kidunia, ikiwemo, uzalishaji kwa viwango bora.
8. Katika shughuli hii ya leo, tumepokea mrejesho mzuri wa kahawa ya Tanzania na maoni ya namna ya kuongeza zaidi soko la kahawa, ambalo kwa namna moja ama nyingine linawagusa wakulima wa Tanzania moja kwa moja katika kuongeza uchumi wao na pato la Taifa kwa ujumla.
9. Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo kwa kuwekeza katika miradi ya muda mrefu na mifupi pamoja na maeneo ya msingi ya kutatua changamoto za kilimo kuanzia shambani hadi sokoni ili kujihakikishia uhakika wa chakula, kulisha wengine kibiashara duniani, lakini pia wakulima kujipatia kipato cha kutosha ili kupunguza umaskini.
10. Aidha, Serikali ya Awamu ya Sita kwa kasi kubwa imewekeza kwenye rasilimali fedha na watu pamoja na uhamasishaji wa sekta binafsi kuwekeza na kukifanya kilimo kuanza kutoa ajira zenye staha hususan, kwa vijana na wanawake, ikiwa ni pamoja na hatua ya kuongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo na kujenga msingi imara wa utekelezaji wa mipango ya kilimo yenye kutazama Tanzania ifikapo mwaka 2050.
11. Nasi Ubalozi tuna jukumu kubwa la kuendelea kutafuta masoko ya bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini ikiwemo, mazao ya kilimo kama kahawa, kwa kutangaza bidhaa hizo na kutafuta wawekezaji katika kuendeleza sekta mbalimbali kama vile sekta ya kilimo hususan, kilimo cha biashara kwa mazao ya kimkakati. Hivyo, nirejee wito wangu kwa watanzania kuzingatia ubora wa viwango katika bidhaa tunazozalisha ili kujihakikishia soko la uhakika kwa wakati wote.
12. Nihitimishe kwa kuwahamasisha wazalishaji, wanunuzi na wasafirishaji wa kahawa ya Tanzania na wadau wengine wote wa mnyororo wa thamani wa zao hili kuja kushiriki kwa wingi katika Maonesho Makubwa ya Kimataifa ya Kahawa ya Mwaka 2023 (World Speciality Coffee 2023) yatakayofanyika jijini Tokyo tarehe 27 -29 Septemba 2023. Bodi ya Kaawa Tanzania inaratibu ushiriki wa Tanzania kama ilivyokuwa mwaka jana. Maonesho haya hutoa fursa muhimu sana kwa wadau wa kahawa duniani kukutana na kubadilishana taarifa muhimu, uzoefu na maarifa kuhusu kahawa.
Domo Arigato Gozaimashta; Asanteni sana kwa mahojiano haya.