Balozi Luvanda kwenye picha ya pamoja na Bw. TAKAGI Kei, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje (Masuala ya Bunge) Japan, aliyekuwa Mgeni Rasmi wa hafla ya Maadhimisho ya Miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, jijini Tokyo.
Balozi Luvanda kwenye picha ya pamoja na Bw. TAKAGI Kei, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje (Masuala ya Bunge) Japan na Bw. Masakatsu Okumoto, Mkurugenzi Mkuu Masuala ya Africa kutoka JICA. Kulia ni Bi. Consolata Lukuvi Luvanda, Mwenza wa Balozi Luvanda.
Balozi Luvanda akitoa salamu za ukaribisho kwa wageni waalikwa waliohudhuria hafla ya Maadhimisho ya Miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Mgeni Rasmi, Bw. TAKAGI Kei, akiwasilisha salamu za pongezi kutoka Serikali ya Japan wakati wa hafla ya Maadhimisho ya Miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Balozi Luvanda akimkabidhi zawadi za Tanzania, Bw. TAKAGI Kei, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje (Masuala ya Bunge) Japan niaba ya Serikali ya Japan wakati wa hafla ya Maadhimisho ya Miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Balozi Luvanda akimkabidhi zawadi za Tanzania, Bw. Masakatsu Okumoto, Mkurugenzi Mkuu Masuala ya Africa wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) wakati wa Maadhimisho ya Miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Baadhi ya wageni waalikwa wakifuatilia filamu yenye kuelezea vivutio vya utalii, fursa za biashara na uwekezaji Tanzania wakati wa Maadhimisho ya Miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, jijini Tokyo.

Katika kuadhimisha Siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa mwaka 2023, Ubalozi uliandaa hafla maalum ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku hiyo muhimu ya Kitaifa, tarehe 26 Aprili 2023, kwenye Hoteli ya Okura, jijini Tokyo. Hafla hiyo ilihudhuriwa na wageni wapatao 120 kutoka Serikali ya Japan, wanadiplomasia wenye uwakilishi nchini Japan, jumuiya za wafanyabiashara na wawekezaji pamoja na viongozi wa Jumuiya ya Watanzania walioko nchini Japan.

Mgeni Rasmi katika hafla hiyo alikuwa Bw. TAKAGI Kei, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje (Masuala ya Bunge) nchini Japan aliyeambatana na viongozi wengine wa wizara hiyo na viongozi wengine kutoka Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA). Aidha, Bw. Tamaki Saito, Naibu Meya wa Jiji la Nagai alihudhuria hafla hiyo akimwakilisha Meya wa jiji hilo, Bw. Shigeharu Uchiya. Tanzania na Mji wa Nagai zimekuwa na ushirikiano uliodumu kwa muda mrefu tangu mwaka 2015 ukiwa na manufaa kwa pande zote mbili kupitia nyanja za kijamii, sanaa, michezo na utamaduni.

Akiwasilisha salamu za ukaribisho kwa wageni waalikwa, Balozi Luvanda alitoa historia fupi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo iliundwa tarehe 26 Aprili, 1964 ikiwa ni Muungano wa Mataifa mawili huru ya Jamhuri yaTanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar yaliyoingia Mkataba wa Muungano mnamo mwaka 1964. Mkataba wa Muungano ulitiwa saini na aliyekuwa Rais wa Tanganyika, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, 22 Aprili 1964 huko Zanzibar; na kuthibitishwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi mnamo tarehe 26 Aprili 1964. Aliuelezea Muungano huo kuwa ni fahari ya watanzania wote na tunu ya kuenziwa iliyodumu kwa miaka 59 tangu kuasisiwa na viongozi wake wa Kitaifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Karume. 

Aidha, Balozi Luvanda katika salamu zake aliishukuru Serikali ya Japan kwa uhusiano mzuri wa kidiplomasia na wa kidugu uliojengeka kwa muda mrefu tangu Tanzania ilivyopata uhuru wake, mwaka 1961. Uhusiano huo uliouwezesha Tanzania kutekeleza miradi yake kimaendeleo pamoja na programu mbalimbali za kukabiliana na umaskini. Alieleza kuwa kupitia uhusiano huo mzuri, Tanzania inamuangalia na kumtambua Japan kama rafiki wa karibu na mdau mkubwa wa maendeleo yake hususan, ya kiuchumi na kijamii. Alitumia fursa hiyo kuwatakia Japan mafanikio katika Mkutano wa Nchi za Kundi la G7 utakaofanyika jijini Hiroshima, tarehe 19 - 21 Mei 2023 ambapo, Japan ni mwenyeji na Rais wa Kundi hilo kwa mwaka 2023.

Balozi Luvanda alihitimisha salamu zake kwa kuwashukuru wageni waalikwa kwa salamu za pongezi na ujio wao ambao umewajumuisha pamoja kuadhimisha siku hiyo ya Kitaifa kwa Tanzania. Alitumia nafasi hiyo pia kumkaribisha mgeni rasmi kutoa salamu zake.   

Kwa upande wake, Bw. TAKAGI Kei, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje (Masuala ya Bunge) Japan, kwa niaba ya Serikali ya Japan alishukuru kwa mwaliko na kuipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutimiza miaka 59 ya Muungano wake. Alielezea historia ya Japan na Tanzania kama mataifa rafiki yaliyoanzisha ushirikiano kwa muda mrefu tangu kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika mwaka 1961. Alimpongeza Balozi Luvanda kwa kazi nzuri ya kuuendeleza na kuudumisha uhusiano huo, kama Balozi wa Tanzania nchini Japan. 

Bw. Kei aliwasilisha salamu za pongezi kwa Rais Samia Suluhu Hassan, na kuuelezea uongozi wa Rais Samia tangu kuingia kwake madarakani mwezi Machi 2021 ambapo alieleza kuwa umeleta mageuzi makubwa nchini katika nyanja mbalimbali hususan, kupitia utekelezaji wa falsafa yake ya 4R’s (Reconsiliation, Resilience, Reform na Rebuild). Aidha, aliishukuru Tanzania kwa ushiriki wake katika Mkutano wa Nane wa Kilele wa TICAD (TICAD 8) uliofanyika mwezi Agosti 2022, Tunisia na katika Hafla ya Mazishi ya aliyekua Waziri Mkuu wa Japan, Hayati Shinzo Abe, mwezi Septemba 2022 nchini Japan; ambapo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa alimuakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika matukio yote mawili.  

Bw. Kei alirejea kuelezea ushirikiano mzuri kati ya Tanzania na Japan uliowezesha kutekelezwa kwa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini Tanzania akitoa mifano ya miradi michache ya miundombinu, elimu na kilimo kuwa imechangia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi wa Tanzania; Mpango wa kuimarisha Uzalishaji wa Mpunga nchini Tanzania ulioanzishwa mwaka 1974 na Serikali ya Japan kupitia Shirika lake la JICA, umesaidia kusambaza teknolojia za kilimo cha mpunga kupitia miradi mbalimbali ikiwemo, Mradi wa Kusaidia Kukuza Sekta ya Mpunga nchini Tanzania (TAN-RICE), Mradi wa Kujenga Uwezo kwa Wataalamu ili Kukuza Maendeleo ya Skimu za Umwagiliaji Chini ya Mipango ya Kilimo ya Wilaya (TANCAID) na Mradi wa Kuendeleza Skimu za Umwagiliaji za Wakulima Wadogo (SSIDP). 

Alieleza kuwa kupitia Mpango wa Uzalishaji Mpunga, Tanzania imekuwa na uwezo wa kuzalisha mchele kwa wingi na kujihakikishia usalama wa chakula ambapo, kwa mwaka 2020/2021 Tanzania imeweza kuzalisha mchele kwa wastani wa tani milioni 1.85; na hivyo kufanya kuwa nchi ya kwanza katika Ukanda wa Afrika Mashariki na miongoni mwa nchi 5 barani Afrika, zinazozalisha mchele kwa wingi. 

Vilevile, Bw. Kei alieleza kuwa makampuni ya Japan yameonesha kuvutiwa na sera rafiki zinazovutia shughuli za biashara na uwekezaji Tanzania, uwepo wa rasilimali za kutosha ikiwemo, ardhi yenye rutuba kwa shughuli za kilimo; madini mbalimbali kama vile cobalt na nickel ambayo mahitaji yake ni mkubwa katika utengenezaji wa mabetri ya vyombo vya moto. Alielezea zaidi kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na vivutio vingi vya utalii ikiwemo, Mlima Kilimanjaro, Visiwa vya Zanzibar na Mbuga ya Wanyama ya Serengeti vimekuwa vivutio vikubwa kwa wajapani wengi na ni matumaini yake kuwa kufuatia kufunguliwa kwa mipaka ya nchi hiyo, wajapani wengi watapenda kuitembelea Tanzania. Pia, alibainisha kuwa uwepo wa asilimia kubwa ya kundi la vijana Tanzania, kunahamasisha Japan kuendeleza programu mbalimbali za ukuzaji shughuli za vijana na maendeleo ya rasilimali watu nchini Tanzania. 

Bw. Kei alihitimisha salamu zake kwa kuihakikishia Serikali ya Tanzania ushirikiano kutoka Serikali ya Japan na kuwa itaimarisha ushirikiano huo kupitia ufuatiliaji na utekelezaji wa yaliyoafikiwa wakati wa Mkutano wa TICAD 8. 

Maadhimisho ya Miaka 59 ya Siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yalipambwa kwa maonesho ya vivutio vya utalii, utamaduni, fursa za biashara na uwekezaji kupitia filamu ya Tanzania – The Royal Tour ambayo imetafsiriwa kwa lugha ya Kijapani; filamu ya uwekezaji iliyoandaliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC); na chapisho maalumu lililoandaliwa na Ubalozi lenye kuelezea kwa pamoja fursa za Tanzania na uhusiano wa Japan: "Tanzania at 59: What Tanzania Wants - A Fresh Look at Tanzania and Japan Relations".

  • Balozi Luvanda kwenye picha ya pamoja na  wawakilishi kutoka asasi za kiraia, jumuiya za wafanyabiashara na wawekezaji wa nchini Japan wakati wa Maadhimisho ya Miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, jijini Tokyo.Balozi Luvanda kwenye picha ya pamoja na wawakilishi kutoka asasi za kiraia, jumuiya za wafanyabiashara na wawekezaji wa nchini Japan wakati wa Maadhimisho ya Miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, jijini Tokyo.
  • Balozi Luvanda kwenye picha ya pamoja na baadhi ya Wanadiplomasia wenye uwakilishi nchini Japan wakati wa Maadhimisho ya Miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.Balozi Luvanda kwenye picha ya pamoja na baadhi ya Wanadiplomasia wenye uwakilishi nchini Japan wakati wa Maadhimisho ya Miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
  • Balozi Luvanda kwenye picha ya pamoja na baadhi ya viongozi  wa Jumuiya ya Watanzania walioko nchini Japan pamoja na watumishi wa Ubalozi wakati wa Maadhimisho ya Miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar jijini Tokyo.Balozi Luvanda kwenye picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Jumuiya ya Watanzania walioko nchini Japan pamoja na watumishi wa Ubalozi wakati wa Maadhimisho ya Miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar jijini Tokyo.