Kampuni mbili za chai za nchini Japan, ITO EN Ltd., na Nasa Corporation zinatarajia kufanya ziara ya siku nne (04) nchini Tanzania ukiwa ni muendelezo wa juhudi za Serikali ya Tanzania kupitia Bodi ya Chai Tanzania (TBT) kuliongezea thamani zao hilo, nchini.

Wakiwa nchini wanatarajiwa kuwa na mazungumzo na wadau mbalimbali wa zao la chai ikiwemo, sekta ya umma na binafsi pamoja na kutembelea mashamba ya chai na viwanda vya kuchakata chai vya Tanzania, kwenye mikoa ya Tanzania inapolimwa chai.

Ziara hii inafuatiwa na matokeo chanya ya ziara iliyofanyika mwezi Disemba 2024 na kampuni za Japan za Kawasaki Kiko na Nasa Corporation ambapo, iliyokuwa timu ya awali ya kufanya tathmini ya zao hilo na baadaye kuishauri Kampuni ya ITO EN ili kutimiza dhamira yake ya kushirikiana na Tanzania (katika uwekezaji na biashara) kwenye zao la chai hususan, chai ya kijani.

Mapema wiki iliyopita, Balozi Baraka Luvanda alifanya mkutano na wawakilishi wa kampuni hizo wanaotarajia kuwasili nchini mnamo tarehe 10 Machi 2025 kwa ajili ya kufanikisha ziara hiyo muhimu. Balozi Luvanda alitumia fursa hiyo kuwatakia kila la kheri katika ziara yao na kuwakaribisha nchini Tanzania; pamoja na kuwaahidi ushirikiano wa Ubalozi na taasisi husika husika za Tanzania katika kutimiza dhamira yao wanayokusudia.