Kampuni ya Tully’s inayomiliki migahawa maarufu ya TULLY’s imezindua rasmi uuzaji wa kahawa ya Tanzania katika migahawa yao yote iliyoko nchini Japan. Uzinduzi huo ulifanyika tarehe 7 Juni 2023; na kufuatiwa na zoezi la uonjaji kahawa iliyozinduliwa ya Tanzania, lililofanyika leo tarehe 9 Juni 2023, katika moja ya mgahawa wao uliopo Tokyo, Japan.
Zoezi hili la uonjaji wa kahawa iliyozinduliwa lilishuhudiwa na Mheshimiwa Balozi Baraka Luvanda, Balozi wa Tanzania nchini Japan; Bw. Daisuke Shindo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mauzo wa Tully’s; Bw. Masahiko Yoshimura, Meneja Mkuu wa Idara ya Bidhaa za Vinywaji wa Kampuni ya Marubeni, ambayo ni mbia wa Tully’s na miongoni mwa kampuni zinazosafirisha kwa wingi kahawa kutoka Tanzania kuingia nchini Japan.
Tully’s Co. Ltd., inamiliki migahawa takribani 700 nchini Japan na imejipatia umaarufu mkubwa katika biashara ya uuzaji wa kahawa za aina mbalimbali duniani. Kahawa ya Tanzania iliyozinduliwa ni kutoka Mashamba ya Kahawa ya GDM (GDM Farms) yaliyoko Mbozi mkoani Mbeya.
Kuzinduliwa kwa kahawa ya GDM nchini Japan kunapandisha zaidi uhakika wa soko la kahawa ya Tanzania nchini Japan ambayo imejizolea umaarufu mkubwa kwa ubora na radha ya aina yake na kupelekea kupewa jina maarufu la kibiashara la Kilimanjaro Coffee. Jina hili hutumika nchini Japan, kwa kahawa zinazozalishwa Tanzania pekee, kwa kutambua kivutio kikubwa cha Mlima Kilimanjaro uliopo nchini Tanzania.
Tanzania inasifika Japan kwa kutoa kahawa bora aina ya Arabica (Arabica laini - full washed na Arabica ngumu - natural) inayolimwa katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Mara, Tanga, Morogoro, Njombe, Iringa, Katavi, Rukwa, Ruvuma, Kigoma, Songwe na Mbeya; na kahawa ya Robusta inayolimwa mkoani Kagera.
Akitoa hotuba yake katika uzinduzi huo, Balozi Baraka Luvanda alizihakikishia kampuni za Japan, uwepo wa mazingira wezeshi ya biashara na hata uwekezaji wanapoamua kuwekeza katika kilimo au sekta nyinginezo. Amelitaja kuwa zao la kahawa ni miongoni mwa mazao ya kimkakati nchini ambalo, linatumika kibiashara kwa kulipatia Taifa pato kubwa kwa mauzo mengi ya kigeni. Akitolea mfano wa Japan, alieleza kuwa kwa mwaka, Tanzania inauza kahawa yake Japan, kwa wastani wa asilimia 33 ya kahawa inayolimwa nchini, ambayo ni sawa na wastani wa kilogramu million 15 (tani 15,000) ya kahawa yote ya Tanzania inayouzwa nchini Japan.
Balozi Luvanda alieleza kuwa soko la kahawa nchini Japan bado ni kubwa, ikilinganishwa na matumizi na uhitaji wa Japan ambapo, Japan uhitaji wake ni wa wastani wa kilogramu milioni 453 (tani 453,000) za kahawa kwa mwaka. Hivyo, Balozi Luvanda alitoa rai kwa watanzania hususan, wakulima wa zao la kahawa, watayarishaji, wasafirishaji na wafanyabiashara wa zao hili kuchangamkia fursa ya soko kubwa la Japan ambalo linakua siku hadi siku.
“Napenda kutoa wito kwa watanzania wenzangu kuzingatia ubora wa viwango kwa mazao tunayolima nchini kwani nchi nyingi tunakouza bidhaa zetu hususan, hapa Japan wanazingatia sana viwango. Hivyo, ili kulikamata soko hili la Japan ipasavyo, inatupasa kwenda sambamba na mahitaji ya kidunia ikiwemo, uzalishaji kwa viwango bora” alieleza Balozi Luvanda.
Aidha, Balozi Luvanda alielezea juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo kwa kuwekeza katika miradi ya muda mrefu na mifupi pamoja na maeneo ya msingi ya kutatua changamoto za kilimo kuanzia shambani hadi sokoni ili kujihakikishia uhakika wa chakula, kulisha wengine kibiashara duniani, na pia wakulima kujipatia kipato cha kutosha ili kupunguza umaskini.
“Serikali ya Tanzania kwa kasi kubwa imewekeza kwenye rasilimali fedha na watu pamoja na uhamasishaji wa sekta binafsi kuwekeza na kukifanya kilimo kuanza kutoa ajira zenye staha hususan, kwa vijana na wanawake, ikiwa ni pamoja na hatua ya kuongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo na kujenga msingi imara wa utekelezaji wa mipango ya kilimo yenye kutazama Tanzania ifikapo mwaka 2050”, alieleza.
Alihitimisha hotuba yake kwa kuelezea jitihada za ubalozi za kufanikisha azma ya Serikali ya Tanzania katika mageuzi ya sekta ya kilimo ya kukifanya kuwa biashara. “Ubalozi unatekeleza jukumu kubwa la kuendelea kutafuta masoko ya bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini ikiwemo, mazao ya kilimo kama kahawa, kwa kuzitangaza bidhaa hizo na kutafuta wawekezaji wa kuendeleza sekta mbalimbali kama vile sekta ya kilimo hususan, kilimo cha biashara kwa mazao ya kimkakati”, alihitimisha.
Mwisho Balozi Luvanda alihamasisha ushiriki wa wadau wa kahawa nchini katika Maonesho ya Kimataifa ya Kahawa ya Mwaka 2023 (World Specialty Coffee Conference and Exhibition 2023) yatakayofanyika jijini Tokyo tarehe 27 – 29 Septemba 2023, ambayo yanaratibiwa na Ubalozi kwa kushirikiana na Bodi ya Kahawa Tanzania. Tanzania ilishiriki kikamilifu katika Maonesho hayo kwa mwaka 2023 na manufaa yake yameonekana.
IMETOLEWA NA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI JAPAN
TAREHE 9 JUNI 2023