HOTUBA YA BALOZI BARAKA H. LUVANDA, BALOZI WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NCHINI JAPAN WAKATI WA SHINDANO LA 34 LA HOTUBA KWA LUGHA YA KISWAHILI LA KUWANIA KOMBE LA MUASISI WA CHUO KIKUU CHA SOKA, DKT. DAISAKU IKEDA
TAREHE  24 NOVEMBA 2024

Ndugu Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha SOKA Mliopo Hapa;
Ndugu  Wageni Mashuhuri Mlioalikwa Mahali Hapa;
Washiriki wote wa Shindano la 34 la  Hotuba ya Kiswahili;
Wanafunzi wote wa Chuo Kikuu cha SOKA mliojumuika hapa;
Ndugu Wageni Wote Waalikwa;
Mabibi na Mabwana.

Jambo? Habari zenu?
Mina-san Konnichi wa!

Naomba nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa wingi wa rehema na baraka zake ambazo zimetuwezesha kukutana hapa leo. Tunamrudishia Mungu sifa na utukufu wake.

Pili, nitoe shukrani zangu za dhati kwa uongozi wa Chuo Kikuu cha SOKA kwa kuendeleza utamaduni wa kuwa na shindano hili kila mwaka ambapo, kwa mwaka huu tunaadhimisha miaka thelathini na nne (34) tangu kuasisiwa kwake.

Na pengine siku ya leo ina umuhimu wa kipekee zaidi kwa kuwa shindano linafanyika mwaka mmoja baada ya Muasisi wa Taasisi hii, Hayati Dkt. Daisaku Ikeda alipofariki Dunia mnamo tarehe 15 Novemba 2023.

Hivyo, wakati tukiendelea kuhunika kwa kifo chake, yatupasa pia kufurahia urithi mkubwa aliotuachia Dkt. Ikeda ambao ni mbegu ya amani aliyoipanda kwa jamii yetu. Ni dhahiri machapisho mengi aliyotuachia katika maktaba ya Chuo Kikuu cha SOKA na sehemu mbali mbali duniani alikofundishwa wakati wa uhai wake yataendelea kuchochea amani na utulivu vinavyoendelea kukumbwa na  misukosuko kila kukicha.


Ndugu Washiriki,
Mabibi na Mabwana,

Naomba pia mniruhusu kutoa shukrani zangu kwa Uongozi wa Chuo Kikuu cha Soka kwa upendeleo mlionipatia wa kunialika kwa mara ya tatu mfululizo kushiriki kama Mgeni Rasmi na  mmojawapo wa Majaji wa Shindano hili. Nawashukuru sana.

Lakini pia, nitumie fursa hii kuwapongeza kwa dhati Waandaaji wa Shindano hili la Kiswahili, Klabu ya Urafiki ya Pan African (Pan African Friendship Society) ya Chuo Kikuu cha Soka, kwa maandalizi mazuri ya mashindano haya. Hongereni sana.

Aidha, nitakuwa nimefanya kosa la kiitifaki nisipowapongeza washiriki wote wa shindano la mwaka huu ambao ndiyo sababu tumekusanyika mahali hapa leo. Hongereni sana kwa bidii kubwa mliyoonesha katika kuandaa hotuba zenu na pia kwa ujasiri na uthubutu wa kushiriki katika shindano.

Tupo hapa leo kuwasikiliza namna mtakavyojieleza kupitia hotuba zenu kwa lugha ya Kiswahili na hatuna shaka yoyote kuhusu umahiri wenu. Zaidi, tuna hamasa kubwa kuwasikia mkibainisha suluhisho za changamoto kubwa zinazoikabili dunia yetu katika nyakati hizi, hususan kukosekana kwa amani.

Ndugu Washiriki,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana,

Maudhui kuu ya Shindano la Hotuba la Mwaka huu imejikita katika amani ya ulimwengu ambapo, “Mambo unayotakiwa kusema kwa lugha ya hekima ni matumaini au matamanio ya kuwa na kesho iliyojazwa tabasamu.”

Maudhui hii inatukumbusha kwamba tunapaswa kutumia lugha inayojumuisha maneno au matamshi yetu kwa hekima na busara kwani yanaweza kuleta athari chanya kwa wengine kama vile; kujenga jamii yenye matumaini na kuacha urithi wa furaha kwa vizazi vijavyo.

Pengine ni sahihi kutumia mfano wa nchi yangu- (Tanzania), ambayo inasifika duniani kwa kutumia lugha yake ya Kiswahili, kama urithi wa vizazi na vizazi kama chombo cha kuleta umoja katika jamii, kuimarisha na kudumisha amani na maelewano miongoni mwa jamii ya watanzania wapatao milioni 61 (Sensa 2022) na makabila yaptayo mia moja na ishrini na sita (126), kila kabila likiwa na lugha yake ya asili.

Ni faraja iliyoje kuona kuwa watanzania wameunganishwa pamoja na lugha ya  Kiswahili ambayo ndiyo Lugha ya Taifa ambapo asilimia 90 ya watanzania wanaizungumza nchini kote.

Muasisi wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Kwanza na Baba wa Taifa la Tanzania alitumia lugha ya Kiswahili kutuunganisha watanzania wote kama watu wa Taifa moja na jamii ya waswahili, hivyo kuepusha hali ya mifarakano na kutoelewana miongoni mwetu.

Aidha, kupitia lugha hii, alitujengea mahusiano bora miongoni mwa jamii ya watanzania; aliwaunganisha watanzania kuwa kitu kimoja wakati wa harakati za kudai uhuru wa kisiasa nchini na katika nchi jirani na Tanzania, akibainisha wazi kuwa wakati wa harakati hizo, “isingekuwa na maana yoyote kwa Tanzania kuwa huru endapo nchi jirani zingeendelea kuwa chini ya ukoloni”. Maneno haya yalikuwa ni chachu na kichocheo  kikubwa kwa Tanzania kusaidia  kwa hali na vitendo katika harakati nyingi za ukombozi, hususan Kusini mwa Afrika.

Hivyo, ndugu zangu kama mada ya leo inavyotukumbusha, lugha au matamshi yenye hekima kama haya ya Hayati Mwalimu Nyerere  yanaweza kuleta mtazamo chanya unaoweza kubadilisha jinsi tunavyochukulia changamoto na kutusaidia kubaki na matumaini hata wakati wa kupitia nyakati ngumu za maisha.


Ndugu Washiriki
Mabibi na Mabwana,

Kwa kutambua mchango mkubwa wa lugha hii ya Kiswahili katika jamii ya wanayoizungumza hususan, katika kuleta umoja mnamo mwezi Novemba 2021, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) liliitangaza tarehe 7 Julai ya kila mwaka ni Siku ya Kiswahili Duniani.

Tarehe hiyo ilichaguliwa mahsusi kwani ndiyo tarehe ya kuzaliwa Chama cha TANU- (7.7.1954) ambacho ndicho kilichopigania uhuru wa Tanzania (wakati huo ikijulikana Tanganyika).

Ubalozi umekuwa ukiandaa siku ya Kiswahili kila mwaka tangu ilipotangazwa na ninapenda kushukuru Chuo Kikuu cha Soka kwa kujumuika nasi wakati wote.

Naomba kutumia fursa hii pia, kutoa rai na kuwahamasisha kuiendeleza lugha hii adhimu kwa kujifunza na kuitangaza kwa umma wa Japan ili ieleweke na kuzungumzwa na wajapani wengi zaidi. Niwahakikishie ushirikiano wa Ubalozi wa Tanzania kwa wakati wote katika kukuza na kukiendeleza Kiswahili nchini Japan.

Ndugu Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana,

Naomba nirejee shukrani zetu kwa kutupatia fursa hii muhimu na adhimu ya kujumuika pamoja nanyi kuadhimisha Shindano la 34 la Hotuba kwa Lugha ya Kiswahili hapa Chuo Kikuu cha Soka.

Ninawatakia washiriki wote kila la kheri katika shindano hili. Kiukweli, binafsi ninawahesabu ninyi nyote washiriki wa shindano hili kuwa ni washindi kwa ule uthubutu wenu tu wa kuingia katika shindano hili la  kuizungumza lugha hii tena kwenye hadhira hii kubwa leo hii. Hivyo, niwatie shime kila mmoja wenu kwa Kiswahili,  jitahidi, utashinda! au kama isemavyo kwa kijapani, Gambare!!!


                  ………………………………………………………………………………
                   


Mungu Ibariki Afrika,
Mungu Ibariki Tanzania,
Mungu Ibariki Japan,
Mungu Ibariki Lugha Yetu  Pendwa ya Kiswahili!
Ahsanteni Sana kwa kunisikiliza!
Domo Arigato Gozaimashta!
 

  • H.E. Ambassador Baraka Luvanda in a group photo with contestant and other invited guests at the 34th Swahili Speech Contest for the Founder’s Cup of Soka University, Dr. Daisaku Ikeda.H.E. Ambassador Baraka Luvanda in a group photo with contestant and other invited guests at the 34th Swahili Speech Contest for the Founder’s Cup of Soka University, Dr. Daisaku Ikeda.