Mhe. Anthony Mavunde (Mb), Waziri wa Madini amekutana na kufanya mazungumzo na Bw. Andrew Spinks, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya EcoGraf ya Australia inayotekeleza mradi wa uchimbaji madini ya graphite katika wilaya ya Mahenge, Morogoro. Kampuni ya EcoGraf imeingia ubia na Serikali ya Tanzania kwa kuunda kampuni iitwayo DUMA ambayo ndio itaendesha mradi huo.

Bw. Spinks aliyeambatana na Bi. Christer Mhingo,  Mkurugenzi wa kampuni ya EcoGraf nchini Tanzania alitumia fursa hiyo kuelezea maendeleo ya kazi walizofanya hadi sasa kuelekea kuanza utekelezaji wa mradi. Aidha, alielezea changamoto kampuni inazokumbana nazo katika kukamilisha taratibu za kuenda kuanza utekelezaji wa  mradi.

Kwa upande wake Mhe. Waziri Mavunde alimshukuru Bw. Spinks kwa kuendelea kuizungumzia vyema Tamzania na kuwa tayari kuwekeza nchini humo. Pia aliwatoa wasiwasi kuhusu changamoto wanazokumbana nazo na kuwaelekeza kufika ofisi za Wizara ya Madini mara moja kwa ajili ya kusaidiwa kutatua. Alimhakikishia Bw. Spinks kuwa Serikali iko tayari muda wote kufanya nao majadiliano ili kukwamua changamoto zao kwa manufaa ya kampuni kwa upande mmoja na Serikali kwa upande mwingine.