Balozi Baraka Luvanda ameagana rasmi na Watanzania waishio Japan (Diaspora) kufuatia kukamilika kwa kipindi chake cha miaka minne cha kutumikia nafasi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Japan.
Katika salamu zake za kuaga, Balozi Luvanda aliwasihi Watanzania hao kuendelea kuishi kwa umoja, mshikamano na mshikikiano, huku wakitii sheria na taratibu za nchi mwenyeji, Japan. Aidha, aliwahimiza kuendelea kuitangaza Tanzania na fursa mbalimbali za kiuchumi, utalii, utamaduni na uwekezaji zinazopatikana nchini, ili kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Japan.
Kwa upande wa viongozi wa Diaspora, salamu za shukrani ziliwasilishwa na Mwenyekiti wa Tanzanite Society (Jumuiya ya Watanzania waishio Japan), Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Kitanzania wanaosoma Japan (TSJ), pamoja na Kapteni wa Timu ya Mpira wa Miguu ya Diaspora ya Tanzania (Kilimanjaro FC). Viongozi hao walimshukuru Balozi Luvanda kwa uongozi wake thabiti akiwa mlezi wao, na kumpongeza kwa mchango wake wa kuwaunganisha Watanzania wote waliopo maeneo mbalimbali ya Japan, na kutambua mchango wao katika Ujenzi wa Taifa.