Tarehe 13 Februari 2026, Mheshimiwa Balozi Anderson Mutatembwa amepokea ugeni wa Bi. Reina Kato, mwakilishi wa Kampuni ya WATATU, taasisi ya Wajapani waliowahi kujitolea nchini Tanzania kupitia Mpango wa Japan Overseas Cooperation Volunteers (JOCVs). Kampuni hiyo inajikita katika utekelezaji wa miradi ya kijamii yenye lengo la kuwawezesha wakulima wadogo, hususan katika Mkoa wa Ruvuma, kwa kuwapatia mafunzo ya kilimo bora, uongezaji thamani wa mazao, na kuimarisha mbinu endelevu za uzalishaji na masoko.

Katika mawasilisho yake, Bi. Reina Kato alieleza kwa kina kuhusu mradi wa WATATU unaolenga kuwasaidia wakulima wadogo kuongeza tija ya uzalishaji, kipato na ustahimilivu wa kilimo kupitia mbinu bunifu, elimu ya kilimo, pamoja na kuunganisha wakulima na fursa za masoko. Alieleza kuwa mradi huo unalenga kuchangia maendeleo ya kilimo shirikishi na endelevu katika ngazi ya jamii, sambamba na kuimarisha mahusiano ya watu kwa watu kati ya Tanzania na Japan.

Aidha, Bi. Kato aliambatana na mwenzake wa JOCVs, Bw. Jun Nishina, ambaye alitambulishwa rasmi kwa Mheshimiwa Balozi. Bw. Jun anajishughulisha na uandishi wa vitabu na kwa sasa yuko katika hatua ya kukitafsiri kitabu chake kwa lugha ya Kiswahili, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza mawasiliano ya kitamaduni na kielimu kati ya mataifa hayo mawili.

Mheshimiwa Balozi alitoa pongezi kwa mchango wa JOCVs na Kampuni ya WATATU katika maendeleo ya jamii nchini Tanzania, hususan katika sekta ya kilimo, na kusisitiza kuwa Ubalozi utaendelea kuthamini na kuunga mkono juhudi zinazolenga kuwawezesha wakulima wadogo na kuimarisha ushirikiano wa kijamii na kiuchumi kati ya Tanzania na Japan.