Tarehe 16 Februari 2026, Mheshimiwa Balozi Anderson Mutatembwa alipokea ugeni wa Bi. Kuniko Shimizu, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Tanzaniaphilia, inayojishughulisha na biashara na utangazaji wa bidhaa za Tanzania, hususan bidhaa za kiutamaduni ikiwemo picha za Tingatinga, vinyago vya Kimakonde, pamoja na mavazi ya asili kama vile kanga, vitenge na Masai shuka.

Katika mazungumzo hayo, Bi. Shimizu alieleza kuwa lengo la ziara yao lilikuwa ni kujitambulisha rasmi kwa Mheshimiwa Balozi pamoja na kuwasilisha shughuli za kampuni yao, ikiwemo uuzaji wa bidhaa za Tanzania na kuitangaza Tanzania kupitia bidhaa zake za kiutamaduni katika soko la Japan, hususan katika ukanda wa Kansai na jiji la Nagoya ambako ndiko makao makuu ya kampuni hiyo yalipo. Alibainisha kuwa Tanzaniaphilia imekuwa jukwaa muhimu la kukuza uelewa wa utamaduni wa Tanzania nchini Japan kupitia maonesho, mauzo ya bidhaa na matukio ya kitamaduni.

Aidha, alieleza kuwa kampuni hiyo imeendelea kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini Japan katika kuandaa semina, maonesho na majukwaa mbalimbali ya kuitangaza Tanzania, yanayojumuisha wadau wa biashara, utamaduni na marafiki wa Tanzania nchini Japan, kwa lengo la kuimarisha mahusiano ya watu kwa watu (people-to-people diplomacy) pamoja na kukuza masoko ya bidhaa za ubunifu kutoka Tanzania.

Kwa upande wake, Mheshimiwa Balozi Mutatembwa alimshukuru Bi. Shimizu kwa juhudi za kampuni ya Tanzaniaphilia katika kuitangaza Tanzania kupitia bidhaa za kiutamaduni na ubunifu, na kusisitiza kuwa mchango huo unasaidia kuimarisha uchumi na utamaduni kati ya Tanzania na Japan. Aidha, aliahidi ushirikiano wa karibu wa Ubalozi katika kuendeleza majukwaa ya utangazaji wa bidhaa za Tanzania nchini Japan, sambamba na kutoa rai ya kuongezwa kwa wigo wa biashara ya bidhaa za ubunifu na za kiutamaduni ili kuwawezesha zaidi wasanii, wabunifu na wazalishaji wadogo wa Tanzania kunufaika na fursa za soko la Japan.