Tarehe 17 Februari 2026, Mheshimiwa Balozi Anderson Mutatembwa alifanya mazungumzo na Bw. Shinichiro Otsuka, Mkurugenzi Mkuu wa Uendeshaji wa Toyota Tsusho Corporation, katika Makao Makuu ya kampuni hiyo jijini Tokyo.

Mazungumzo hayo yaliambatana na wasilisho la kampuni kuhusu shughuli zake katika mataifa mbalimbali duniani, ikiwemo Tanzania, ambapo imekuwa ikijihusisha na utekelezaji wa miradi katika sekta za usafirishaji, nishati, maji, kilimo, pamoja na maendeleo ya miundombinu rafiki kwa mazingira (green infrastructure). Wasilisho hilo liliainisha dhamira ya kampuni kuendeleza uwekezaji endelevu na miradi ya ubia inayochangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Katika mazungumzo hayo, Bw. Otsuka aliomba ushirikiano wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuendeleza na kuongeza wigo wa shughuli za kampuni hiyo nchini, sambamba na kuonesha utayari wa kushirikiana na Tanzania katika kuibua na kutekeleza miradi mipya ya ubia kwa manufaa ya pande zote mbili, hususan katika sekta za usafirishaji, nishati na maji.

Kwa upande wake, Mheshimiwa Balozi Mutatembwa aliishukuru Toyota Tsusho Corporation kwa ushirikiano wao endelevu na Tanzania katika sekta za afya, kilimo na maendeleo ya miundombinu rafiki kwa mazingira, ikiwemo utekelezaji wa miradi ya usafirishaji, maji na nishati. Aidha, alitumia fursa hiyo kuwahakikishia ushirikiano wa Serikali katika utekelezaji wa shughuli zao nchini, hususan utekelezaji wa Hati za Ushirikiano (MoU) zilizosainiwa hivi karibuni kati ya kampuni hiyo na taasisi za Serikali.

MoU hizo ni pamoja na: Hati ya Ushirikiano kati ya Toyota Tsusho na Bodi ya Pamba Tanzania kuhusu uendelezaji na uongezaji thamani wa mnyororo wa zao la pamba, iliyosainiwa mwezi Julai 2025; na Hati ya Ushirikiano na Wizara ya Uchukuzi kuhusu ushirikiano katika masuala ya usafirishaji, iliyosainiwa pembezoni mwa mkutano wa Tokyo International Conference on African Development (TICAD 9) jijini Yokohama mwezi Agosti 2025.

Pande zote mbili ziliahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kimkakati, kubadilishana taarifa za kiufundi na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya pamoja iliyoainishwa katika MoU, pamoja na kuchunguza fursa mpya za uwekezaji zitakazochangia maendeleo endelevu ya Tanzania, hususan katika sekta za usafirishaji, nishati safi, maji na kilimo.