Tarehe 6 Februari 2026, Mheshimiwa Anderson Mutatembwa alitembelea Kiwanda cha Kuchakata na Kuteketeza Taka cha Kanazawa kinachosimamiwa na Ofisi ya Jiji la Yokohama, na kujionea namna mifumo ya kisasa ya usimamizi wa taka inavyotekelezwa kwa kuzingatia viwango vya juu vya ulinzi wa mazingira na afya ya jamii.
Ziara hiyo kiwandani hapo ilitoa uelewa mpana kuhusu mbinu za uchambuzi na uchakataji wa taka, ikiwemo utenganishaji wa taka katika chanzo, matumizi ya teknolojia ya kuchoma taka (incineration) kwa uzalishaji wa nishati (waste-to-energy), pamoja na mifumo ya kudhibiti hewa chafu ili kupunguza athari za kimazingira. Uzoefu huo unaonesha fursa kubwa ya kujifunza na kubadilishana utaalamu kati ya Jiji la Yokohama na Jiji la Dar es Salaam, hususan katika kuboresha mifumo ya ukusanyaji, uchakataji na uendelezaji wa dhana ya uchumi mzunguko (circular economy).



