Tarehe 11 Februari 2026, Balozi Anderson Mutatembwa amepokea Ujumbe wa Tanzania uliopo nchini Japan kwa majadiliano ya Mkataba wa Uwekezaji (Bilateral Investment Treaty – BIT) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Japan. Ujumbe huo umeongozwa na Balozi Prof. Kennedy Godfrey Gaston (Chief Negotiator) kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki; wajumbe wengine ni maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje pamoja na wizara na taasisi zingine za kisekta ikiwemo, uwekezaji, masuala ya fedha na sheria. 

Ujumbe ulieleza kuwa majadiliano hayo ni mwendelezo wa raundi ya saba ya mazungumzo kati ya pande hizo mbili, yakilenga kufikia makubaliano yatakayochochea, kuwezesha na kulinda uwekezaji kati ya Tanzania na Japan. Raundi ya mwisho ya majadiliano ya ana kwa ana ilifanyika mwaka 2018, huku raundi ya sita ikifanyika kwa njia ya mtandao mwaka 2025 kwa lengo la kufufua mazungumzo hayo.

Katika kikao hicho cha mapokezi, Balozi Mutatembwa alieleza umuhimu wa majadiliano hayo kwa maendeleo ya uchumi wa Tanzania, hususan katika kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka Japan (FDI), kuimarisha mazingira ya biashara na kuongeza ushirikiano wa kimkakati kati ya sekta binafsi za nchi hizo mbili. Aidha, alisisitiza kuwa msimamo wa Tanzania ni kuhakikisha uwekezaji wote unazingatia sheria na sera za nchi, huku ukilinda maslahi ya Taifa na kutoa uhakika (predictability and stability) kwa wawekezaji.

Kwa upande wake, Ujumbe wa Tanzania ulieleza kuwa masuala yanayotarajiwa kujadiliwa kwa kina ni pamoja na tafsiri ya “uwekezaji”, utaratibu wa utatuzi wa migogoro, athari za Sheria za Maliasili ya Mwaka 2017, pamoja na masuala ya vivutio vya uwekezaji na misamaha ya kodi. Ujumbe ulisisitiza kuwa Tanzania inaendelea kuboresha mfumo wake wa kisheria na kiutawala ili kuhakikisha uwekezaji unalindwa chini ya mfumo wa sheria za nchi kwa uwazi, usawa na uendelevu.

Majadiliano hayo yanatarajiwa kuimarisha zaidi uhusiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Japan pamoja na kufungua fursa mpya za uwekezaji katika sekta za kimkakati zikiwemo, nishati, viwanda, kilimo na miundombinu.