Tarehe 13 Februari 2026, Mheshimiwa Balozi Anderson Mutatembwa alifanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tokushukai Medical Group, Bw. Higashiue Shinichi, yaliyojikita katika kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na taasisi hiyo katika sekta ya afya, hususan katika eneo la magonjwa ya figo na upandikizaji wa viungo.
Mazungumzo hayo yalifanyika kwa lengo la kujadili Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Upandikizaji Figo, unaotekelezwa kwa ubia kati ya Tokushukai Medical Group na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Hospitali ya Benjamin Mkapa na Chuo Kikuu cha Dodoma. Mradi huo unalenga kuimarisha upatikanaji wa huduma za kibingwa za upandikizaji figo nchini na kupunguza utegemezi wa rufaa za matibabu nje ya nchi.
Katika mazungumzo hayo, Bw. Higashiue alieleza matarajio yake kuwa Kituo kinachotarajiwa kujengwa kitatoa huduma za upandikizaji figo kwa viwango vya kimataifa, huku mpango wa muda mrefu ukiwa ni kupanua wigo wa huduma ili kujumuisha upandikizaji wa viungo vingine, sambamba na kuwekeza katika ujenzi wa uwezo kwa wataalamu wa afya wa Tanzania na kuimarisha tafiti za kitabibu. Alibainisha kuwa ujenzi wa Kituo unatarajiwa kuanza mwaka huu na kukamilika ndani ya kipindi cha miaka miwili.
Aidha, alisisitiza dhamira ya Tokushukai kuona Kituo hicho kinakuwa Kituo Bobezi cha Kikanda kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, kitakachotoa huduma si kwa Tanzania pekee bali pia kwa nchi nyingine za Afrika, hivyo kuchangia katika kuimarisha diplomasia ya afya na ushirikiano wa kimataifa.
Kwa upande wake, Mheshimiwa Balozi alitoa shukrani za dhati kwa uongozi wa Tokushukai Medical Group kwa ushirikiano wao endelevu na mchango wao mkubwa katika maendeleo ya sekta ya afya nchini Tanzania. Aidha, alimuarifu Mwenyekiti kuhusu Maadhimisho ya Miaka 10 ya Hospitali ya Benjamin Mkapa yanayotarajiwa kufanyika mwezi Mei 2026, na kueleza matarajio ya kuendeleza ushirikiano huo katika hatua zinazofuata.
Mheshimiwa Balozi aliahidi kuwa Ubalozi utaendelea kutoa ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha utekelezaji wa wakati wa mradi huo wa kimkakati kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania na ukanda mzima.



