Tarehe 10 Februari 2026, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Japan, Mheshimiwa Anderson Mutatembwa, alifanya mazungumzo na Rais wa The Association of African Economy and Development in Japan (AFRECO), Bw. Tetsuro Yano, katika Makao Makuu ya Taasisi hiyo jijini Tokyo. Mazungumzo yalilenga kuimarisha na kuongeza wigo wa ushirikiano kati ya Tanzania na AFRECO, hususan katika sekta za afya, elimu ya juu, kilimo, nishati, na maendeleo ya jamii, pamoja na kujadili fursa za utekelezaji wa miradi ya kijamii yenye athari chanya ya moja kwa moja kwa wananchi.
Katika mazungumzo, Bw. Yano alieleza dhamira ya AFRECO ya kuendeleza ushirikiano wake wa muda mrefu na Tanzania. Alisisitiza mchango wa taasisi hiyo katika sekta ya afya nchini Tanzania, hususan kupitia ushirikiano na Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), ikiwemo utekelezaji wa Mradi wa Kituo cha Upandikizaji Figo kwa kushirikiana na taasisi ya TOKUSHUKAI ya Japan, pamoja na kuanzisha Diagnostic Imaging Centre na uendelezaji wa mafunzo ya Biomedical Engineering kwa kushirikiana na JICA, yanayosubiri idhini ya mitaala kutoka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).
Aidha, Bw. Yano alieleza kuwa AFRECO ina dhamira ya kuendeleza miradi mingine ya ushirikiano na Tanzania ikiwemo miradi ya kilimo, hususan majaribio ya matumizi ya viambato vya kuboresha rutuba ya udongo kwa wakulima wadogo kupitia UDOM; miradi ya nishati jadidifu, ikiwemo miradi ya umeme wa maji kwa mfumo wa ubia (PPP); pamoja na uwezekano wa kusaidia upatikanaji wa vifaa vya kilimo vilivyotumika lakini vilivyo katika hali nzuri kwa wakulima wadogo nchini Tanzania.
Balozi Mutatembwa alitumia fursa hiyo, kumshukuru Bw. Yano na taasisi yake kwa mchango wao mkubwa katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini Tanzania, na kueleza dhamira ya Serikali ya kuendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi hiyo katika kufanikisha utekelezaji wa miradi inayolenga kuleta maendeleo ya moja kwa moja kwa wananchi.



