Tarehe 22 Aprili 2026, Ubalozi ulipokea ujumbe wa wawakilishi watatu kutoka Yokohama, ulioongozwa na Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa wa jiji hilo, Bi. Maruyama Akiko. Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kuendeleza majadiliano kuhusu kuanzisha ushirikiano kati ya Jiji la Yokohama na Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo, ujumbe wa Yokohama ulikumbushia maendeleo yaliyofikiwa katika rasimu ya Hati ya Ushirikiano (Memorandum of Understanding – MoU) kati ya majiji hayo mawili. Aidha, waliwasilisha ombi la kuandaliwa kwa mazungumzo ya awali kati ya wataalamu wa Dar es Salaam na Yokohama, kwa lengo la kujitambulisha, kubadilishana uzoefu, pamoja na kubaini maeneo ya kipaumbele kwa ajili ya ushirikiano huo.
Mazungumzo hayo yanatarajiwa kuweka msingi imara wa ushirikiano wa muda mrefu kati ya majiji hayo mawili, hususan katika maeneo ya maendeleo ya miji, miundombinu, mazingira na huduma za jamii.
Ubalozi ulieleza utayari wake wa kuendelea kuratibu na kusaidia juhudi hizo ili kuhakikisha ushirikiano huo unatekelezwa kwa mafanikio na kuleta manufaa kwa pande zote mbili.



