Tarehe 15 Aprili 2026, Ubalozi ulipokea Ujumbe kutoka Japan International Cooperation Agency (JICA) kwa lengo la kumtambulisha Bi. Kana Matsuzaki, Afisa Mshauri wa JICA wa masuala ya utalii endelevu ambaye ataanza rasmi majukumu yake mwezi Mei 2026 katika Wizara ya Utalii na Urithi ya Zanzibar kwa kipindi cha miaka miwili.

Katika mazungumzo hayo, ujumbe wa JICA ulieleza kuwa jukumu la mtaalamu huyo litajikita katika kuimarisha uwezo wa taasisi za utalii Zanzibar, kukuza ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, pamoja na kusaidia kuandaa mikakati na ramani ya utekelezaji wa miradi ya muda mfupi itakayochochea maendeleo ya utalii endelevu. Aidha, alieleza dhamira yake ya kujifunza kwa kina mazingira ya sekta ya utalii Zanzibar ili kubaini maeneo ya kipaumbele yatakayohitaji maboresho na kuanzisha programu za mafunzo kwa wadau husika.

Ubalozi uliukaribisha ujio wa mtaalamu huyo na kueleza matarajio makubwa kuwa uwepo wake utaongeza nguvu katika kuimarisha ushirikiano wa maendeleo kati ya Tanzania na Japan, hususan katika sekta ya utalii Zanzibar. Ubalozi ulisisitiza umuhimu wa kuzingatia utalii endelevu sambamba na fursa zilizopo katika uchumi wa buluu, ikiwemo uvuvi wa bahari kuu, maendeleo ya bandari, pamoja na uwekezaji wa kimkakati unaohusiana na sekta ya utalii.

Mazungumzo hayo pia yaligusia mafanikio ya Zanzibar kama moja ya vivutio vikubwa vya utalii barani Afrika, hususan kutokana na fukwe zake, urithi wa kihistoria wa Stone Town, pamoja na mchango mkubwa wa sekta hiyo katika uchumi wa Zanzibar. Pande zote mbili zilikubaliana kuhusu umuhimu wa kujifunza kutoka uzoefu wa Japan katika usimamizi wa utalii endelevu, hasa kutokana na ongezeko la watalii wa kimataifa nchini humo.

Aidha, pande hizo zilijadiliana kuhusu maandalizi ya ujumbe wa viongozi kutoka Zanzibar kutembelea Japan mwezi Septemba 2026 kupitia mpango wa kuhamasisha uwekezaji, ambapo maeneo ya utalii na uchumi wa buluu yanatarajiwa kupewa kipaumbele. Ilielezwa kuwa ziara hiyo inaweza kujumuisha Mkoa wa Okinawa kutokana na mfanano wake wa kijiografia na Zanzibar, jambo litakalotoa fursa ya kubadilishana uzoefu wa maendeleo ya visiwa vya utalii.

Ubalozi uliahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu na JICA pamoja na mtaalamu huyo katika jitihada za kuitangaza Zanzibar kama kivutio cha utalii na uwekezaji, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa diplomasia ya uchumi.