Tarehe 28 – 29 Juni, 2025 Timu ya wanawake ya Tanzania ya Softball chini ya miaka 18 ilishiriki Mashindano ya Kimataifa ya Kombe la Utsugi “Utsugi Cup International Women’s U-18 Softball Tournament 2025” yaliyofanyika katika uwanja wa Utsugi Stadium uliopo katika mji wa Takasaki Mkoa wa Gunma nchini Japan.
Masindano hayo huandaliwa na Kamati ya Maandalizi ya Kombe la Utsugi chini ya Mwenyekiti wake Mitsuru Uchiyama na Makamu wa Rais wa chama cha softball Takasaki Taeko Utsugi ambaye pia ndiyo mdhamini wa mashindano hayo. Mashindano hayo yaliyofunguliwa na Balozi wa Tanzania nchini Japan Balozi Baraka Luvanda yalijumlisha timu za wanawake chini ya miaka 18 kutoka Japan, Italia, Ujerumani, Tanzania, Singapore na Botswana.
Katika mashindano hayo yaliyofanyika kwa siku mbili, Japan iliibuka msindi kwa kuifunga Italia point 10 kwa 0 katika mchezo wa fainali. Aidha Tanzania walishinda mchezo mmoja dhidi ya Botswana na kuwaweka nafasi ya tano kati ya sita. Mshindi wa pili alikuwa Italia, Ujerumani walishika nafasi ya tatu, Singapore nafasi ya nne na Botswana nafasi ya sita. Timu ya Tanzania yenye jumla ya wachezaji 16 na viongozi 6 imeshiriki kwa mara ya pili mashindano hayo ambapo mara ya kwanza ilishiriki mwaka 2023. Mashindano ya kombe la Utsugi hufanyika kila baada ya mwaka mmoja. Timu ya Tanzania inayoongozwa na Rais wa Chama cha mchezo huo “Tanzania Baseball and Softball Association – TaBSA” Bi. Faraja Robert bado ipo nchini Japan kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii na maonesho ya Dunia ya Osaka 2025 (Osaka EXPO 2025) na wanatarajia kuondoka tarehe 06 Julai, 2025.