Leo tarehe 22 Septemba 2022, Tanzania imezindua rasmi filamu ya The Royal Tour iliyotafsiriwa Kijapan wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Japan yajulikanayo kama Japan Tourism Expo. Maonesho haya ya kimataifa ya utalii Japan yameandaliwa na Taasisi ya Utalii ya Japan, yameshirikisha na kuhudhuriwa na nchi mbalimbali duniani pamoja na wataalamu wa sekta ya utalii duniani kote. Wadau wa utalii pamoja na umma wa Wajapani wanatarajiwa kushiriki maonesho haya yanayofanyika kwa muda wa siku 4.  

Banda la Tanzania limevutia wageni wengi kutokana na vivutio vilivyopo Tanzania ambao wengi wa wageni hao walipenda kuifahamu Tanzania zaidi kupitia vivutio vyake vya asili vya utalii na utamaduni. Wageni hao walipata fursa ya kupokea maelezo kuhusu Tanzania kwa kuanzia historia, uchumi, utamaduni, vyakula na vivutio vilivyopo vya utalii na utamaduni. Wageni pia walipata fursa ya kuonja vivywaji kutoka Tanzania (mvinyo na kahawa) pamoja na kula vyakula vya kitanzania. 

Balozi Luvanda katika hotuba yake alichukua nafasi hiyo kuvielezia vivutio vya utalii vya Tanzania, zikiwepo mbuga za wanyama, Hifadhi za Taifa za wanayamapori, milima na fukwe za kuvutia; aliwasihi waweze kuangalia makala ya filamu inayoitangaza Tanzania, ya “The Tanzania Royal Tour” ambayo kwa siku ya leo filamu hiyo iliyotafsiriwa kwa lugha ya Kijapani imezinduliwa rasmi.  

Balozi Luvanda aliwaeleza kuwa tukio hili limefanyika kipindi kizuri ambapo dunia inaanza kufunguka kufuatia kupungua kwa maabukizi ya virusi ya Corona na hivyo masharti ya kusafiri kutoka nchi moja kuingia nyingine kupungua. Hivyo ni matumaini yake kuwa wageni hao watapanga kutembelea Tanzania kujionea yale yote waliyoelezwa na kujionea wakati wa Maonesho hayo. 

Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Japan yamehudhuriwa na taasisi za utalii za Tanzania ikiwemo, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS). Maonesho haya yatahitimishwa tarehe 25 Septemba 2022, yatatoa fursa kwa wajapani kutalii maeneo mbalimbali duniani ikizingatiwa kuwa Japan sasa imeanza kuruhusu raia wake kutoka nje ya Japan kufuatia kupungua kwa athari za UVIKO – 19. 

  • Mhe. Balozi Baraka Luvanda  kwenye Banda la SADC kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya JapanMhe. Balozi Baraka Luvanda kwenye Banda la SADC kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Japan