Leo, tarehe 1 Julai 2025, Mhe. Balozi Baraka Luvanda amepokea Ujumbe kutoka Ofisi ya Sera ya Afya (Healthcare Policy) ya Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri la Serikali ya Japan. Lengo la ujio wa Ujumbe huo ni kujitambulisha pamoja na kumshirikisha Mhe. Balozi kuhusu maandalizi ya Mkutano Maalum wa Afya utakaofanyika wakati wa TICAD 9 (TICAD 9 Summit) mwezi Agosti, 2025, jijini Yokohama, Japan.

Katika mazungumzo yao, Ujumbe huo ulieleza dhamira ya Serikali ya Japan katika kutekeleza Mpango wa “African Health and Wellbeing Initiative” (AfHWIN) unaolenga kuendeleza jamii yenye afya njema na maisha bora barani Afrika, kupitia ushirikiano na makampuni ya huduma za afya na tiba kutoka Japan.

Aidha, Ujumbe huo ulirejea Hati ya Ushirikiano (MOC) kuhusu AfHWIN iliyosainiwa kati ya Serikali za Japan na Tanzania mnamo mwaka 2019, ambayo ilihuishwa na kuongezwa muda wake mwaka 2024, kwa madhumuni ya kuendeleza ushirikiano baina ya pande mbili katika sekta ya afya.
Kwa muktadha huo, Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri la Japan inaandaa Mkutano huo maalum wa masuala ya afya utakaobeba mada mahsusi kuhusu mafanikio ya Serikali na sekta binafsi ya Japan kupitia mpango wa AfHWIN.

Ujumbe huo pia ulieleza dhamira yake ya kushirikiana kwa ukaribu na Tanzania kwenye maandalizi ya Mkutano huo kwa mada inayohusu utekelezaji wa Tanzania katika Mpango wa AfHWIN ikiwa sehemu ya agenda ya TICAD 9.