Leo, tarehe 27 Juni 2025, Mheshimiwa Balozi Baraka Luvanda ametembelewa na wanafunzi sita kutoka Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) waliokuwa nchini Japan kwa ziara ya mafunzo ya wiki mbili, wakiambatana na walimu wao wawili pamoja na mwakilishi kutoka Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japani (JICA).

Ziara hiyo, iliyoandaliwa kwa lengo la kuwajengea uwezo vijana wa Kitanzania kupitia uzoefu wa moja kwa moja wa teknolojia ya hali ya juu, imehusisha mafunzo ya vitendo na masomo katika Shule ya Ufundi ya Nagai, yenye umaarufu katika fani za mitambo na elektroniki.

Katika mazungumzo yake na ujumbe huo, Mheshimiwa Balozi aliwatia moyo wanafunzi hao kuendelea kujituma katika masomo yao na kutumia vyema maarifa waliyopata kama msingi wa mafanikio yao ya baadaye na mchango wao kwa maendeleo ya taifa. Aidha, aliwasihi kuwa mabalozi wa mabadiliko na mfano kwa vijana wenzao nchini Tanzania.

Pia, alitumia fursa hiyo kupongeza uhusiano wa karibu uliopo kati ya Tanzania na Jiji la Nagai, kupitia ushirikiano wa miji ya urafiki kati ya Jiji la Dodoma na Jiji la Nagai. Ushirikiano huu umeendelea kuimarika kupitia utekelezaji wa programu mbalimbali za elimu, michezo, na utamaduni, unaolenga kujenga uelewa wa pamoja, mshikamano na maendeleo ya kijamii kwa pande zote mbili.

Wakiwa nchini Japan, wanafunzi hao pia walipata fursa ya kukutana na Bwana Naoki Yanase, Mkurugenzi Mkuu wa Kitengo cha Afrika - JICA, ambaye alieleza dhamira ya kuendeleza Mpango huu kwa kuleta kundi jingine la wanafunzi kutoka Tanzania kati ya mwezi Oktoba na Novemba 2025.

Ziara hii ni sehemu ya programu za kuimarisha elimu ya ufundi nchini Tanzania kupitia ushirikiano wa kimkakati kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Japan.