Tarehe 30 Juni 2025, Mheshimiwa Balozi Baraka Luvanda ametembelewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Ubongo na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI), Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya.
Katika mazungumzo yao, viongozi hao walijadili kwa kina fursa mbalimbali zinazoweza kuendelezwa kupitia ushirikiano kati ya Tanzania na Japan, hususan katika kuvutia wawekezaji katika nyanja za upasuaji wa neva (neurosurgery), mifupa (orthopedic) na huduma za kurejesha afya ya viungo (rehabilitation). Japan ikiwa ni miongoni mwa nchi zinazoongoza duniani kwa teknolojia ya kisasa katika sekta ya afya, imeoneshwa kuwa na nafasi muhimu katika kuimarisha uwezo wa MOI kupitia ushirikiano wa kitaalamu, uhamisho wa teknolojia na uwekezaji wa moja kwa moja.
Aidha, Dkt. Mpoki na Ujumbe wake wapo nchini Japan kushiriki Maonesho ya Dunia ya Osaka EXPO 2025, katika Wiki Maalum ya Afya (Health Theme Week), ambapo pamoja na kushiriki midahalo ya kimataifa, amefanikisha pia kufanya mazungumzo na taasisi mbalimbali za afya, ikiwemo hospitali mashuhuri ya FUJITA – inayotambulika kwa ubobezi wake katika teknolojia ya tiba na huduma za afya ya kibingwa. Ushiriki wake katika wiki hii umetoa fursa ya kipekee kwa Tanzania kujifunza, kushirikiana na kuvutia wawekezaji wa sekta ya afya kutoka Japan.




